Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Mkoani leo imezindua rasmi kampeni siku 4 ya utoaji wa Chanjo ya matone ya Polio awamu ya nne ambapo jumla ya watoto 135,615 wenye umri chini ya miaka mitano wanatarajiwa kupatiwa chanjo hiyo.
Akizindua kampeni hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Binuru Shekidele amewataka wazazi na walezi wote wenye watoto walio chini ya miaka mitano kuhakikisha watoto hao wanapatiwa chanjo ya matone ya Polio katika vituo vya kutolea huduma za afya na majumbani ambapo watoa huduma watapita.
"Suala la kupatiwa chanjo ya matone ya Polio si la hiari ni la lazima, hivyo wazazi na walezi hakikisheni watoto wenu wanapatiwa chanjo hii kinyume na hapo tutawachukulia hatua kali wazazi wote watakaoshindwa kuwapeleka watoto kupata chanjo kwani takwimu zote za watoto wenye sifa za kupatiwa Chanjo hii tunazo " alisisitiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji amewashukuru wazazi na walezi wote waliojitokeza kwa ajili ya chanjo hiyo ambapo amesema kwa kufanya hivyo ni kulisaidia taifa katika kupunguza magonjwa ambayo yanaweza kuzuilika.
Naye msimamizi wa chanjo ngazi ya Mkoa Dkt. Saula Beichumila amesema chanjo hiyo ya awamu ya nne kitaifa ni mhimu sana kwa watoto kwani ndiyo hutengeneza kinga mwilini ya ugonjwa wa Polio hivyo amesisitiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wenye sifa wanapatiwa chanjo hiyo.
Kampeni ya Chanjo ya Polio awamu ya nne imezinduliwa kwenye kituo cha afya cha Sengerema ambapo Chanjo hii itatolewa kwenye vituo vyote vya kutole huduma za afya na majumbani. Kampeni hii itahitimishwa siku ya jumapili tarehe 04 Disemba, 2022.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.