Mwenyekiti wa Halmashauri ni Kiongozi Mkuu wa Halmashauri mwenye dhamana ya kisiasa. Dhamana hii humfanya kuwa kioo ndani na nje ya Halmashaui yake.
Mwenyekiti wa Halmashauri ni Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani na Kamati ya Kudumu ya Fedha na Mipango/Utawala.
Kwa mujibu wa Kifungu Na. 193 (2) cha Sheria Na. 7 ya 1982 na Kifungu Na. 108 (2) cha Sheria Na. 8 ya 1982, Mwenyekiti wa Halmashauri ni mtia lakiri/mhuri katika nyaraka zote rasmi za Halmashauri.
Meya/Mwenyekiti wa Halmashauri analo jukumu maalum la kudhibiti na kuongoza mikutano ya Baraza la Madiwani ili liweze kufanya maamuzi yenye maslahi kwa wananchi wote wa Halmashauri. Katika kutimiza jukumu hili Mwenyekiti wa Halmashauri anatakiwa kutenda haki kwa Madiwani wote bila kujali itikadi za Kisiasa, Jinsia, Dini, Rangi au Kabila na wakati wote awe mtulivu, imara na asiyeonyesha udhaifu wakati wa kuendesha vikao.
Ili kutimiza wajibu wake wa Uongozi ipasavyo, Mwenyekiti wa Halmashauri anatakiwa kupewa Ofisi na Halmashauri ambayo ataitumia kukutana na wananchi wote wenye shida, kero na maoni ya kuboresha utendaji wa Halmashauri mara mbili kwa wiki. Ratiba ya siku hizi mbili lazima iwe wazi na ifahamike kwa wananchi wote. Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri kama atataka kutembelea Halmashauri yake katika harakati za kuhimiza maendeleo, atalazimika kufanya kazi hiyo katika siku hizo mbili tu zilizoruhusiwa na sio vinginevyo.