*Mashamba ya Shule Yatumike kwa ajili ya Chakula cha Wanafunzi
Watendaji wa kata za Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema wametakiwa kutoa kipaumbele elimu ya lishe katika jamii hususan suala la wazazi kuchangia chakula katika shule wanazosoma watoto wao ili kufanikisha suala la kuboresha hali ya lishe na kupunguza athari za utapiamlo katika jamii.
Agizo hilo limetolewa leo na Katibu Tawala Wilaya ya Sengerema, Curthbert Midala kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya kwenye kikao cha kamati ya lishe kwa ajili ya kujadili taarifa za kipindi cha Mwezi Julai hadi Septemba 2024 kilichofayika kwenye ukumbi wa Sengerema Sekondari.
Katibu Tawala amesema elimu ya Lishe katika jamii inapaswa kupewa kipaumbele ili jamii iweze kubadilika na kuwa na mtizamo chanya kwenye suala zima la lishe.
"Suala la lishe linapaswa kuzingatiwa na kuwa agenda zenu za kila siku, hata sisi kwenye vikao vyetu, lishe ni agenda ya kudumu" amesisitiza Katibu Tawala.
Kwa upande mwingine Katibu Tawala amewataka watendaji kuendelea kuhamasisha wazazi na walezi wa wanafunzi kuendelea kuchangia chakula kwenye shule wanazosoma watoto wao pamoja na kuhakikisha wanasimamia maadhimisho ya siku ya lishe katika vijiji ili jamii iweze kupata uelewa wa masuala ya lishe ambapo itasaidia kubadili tabia na mitizamo juu ya lishe.
Katika kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni, Katibu Tawala ameagiza mashamba yote yanayomilikiwa na shule yatumike kwa ajili ya manufaa ya wanafunzi ambapo pia ameshauri kutoa motisha kwa kata zinazofanya vizuri kwenye viashiria na malengo ya lishe.
Mapema akitoa maelezo mafupi ya kikao hicho, Mganga Mkuu wa Halmashauri, Fredrick Mugarula amesema Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema inafanya vizuri kwenye malengo 13 ya Lishe ambapo amesema eneo ambalo limekuwa na changamoto ni utoaji wa chakula shuleni pamoja na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya shughuli mbalimbali za lishe.
Wakichangia katika kikao hicho, Watendaji wa kata wamesema wazazi na walezi wamekuwa wagumu kuchangia vyakula shuleni kutokana na sababu mbalimbali, hivyo wameomba uongozi wa Wilaya uweze kutoa tamko ili jamii ilazimike katika uchangiaji wa vyakula shuleni.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.