Milioni 436 Kutolewa na Halmashauri kwa vikundi
Wasimamizi wa Vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ngazi ya kata zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wameaswa kusimamia vyema vikundi vinavyopatiwa mikopo itokanayo na asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri ili mikopo hiyo ilete tija na kuwa na vikundi endelevu.
Wito huo umetolewa leo Oktoba 21, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya utoaji na usimamizi wa mikopo ya asilimia kwa maafisa maendeleo ya jamii kata, polisi kata na watendaji wa kata yaliyofanyika chuo cha maendeleo ya wananchi Sengerema.
Mkuu wa Wilaya amesema kumekuwa na vikundi vingi vinavyokopeshwa na Halmashauri lakini vimekuwa havifanyi vizuri kutokana na kutokuwa na usimamizi mzuri wa matumizi ya fedha, kusuasua kwenye marejesho pamoja na kutokuwa na miradi yenye uhakika hivyo amewataka wataalamu hao kwenda kusimamia vyema vikundi ili mikopo hiyo itakapoanza kutolewa iweze kuvinufaisha vikundi hivyo.
"Mimi nawaomba tuwe sehemu ya mafanikio ya vikundi hivi, Serikali inatoa fedha nyingi sana, tusiwape mikopo watu watakaotuharibia, kuweni sehemu ya mafanikio ya vikundi hivi" amesema Mkuu wa Wilaya.
Mapema akimkaribisha Mkuu wa Wilaya, kaimu Mkuu Mkurugenzi wa Halmashauri Wilbard Bandola amesema Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kwa kipindi itatoa mikopo kwa vikundi vyenye sifa na vilivyokidhi vigezo vilivyowekwa na Serikali hivyo amewaomba wasimamizi hao kuhakikisha wanasimamia vyema sheria na taratibu katika upatikanaji wa vikundi hivyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema baada ya kurejesha utoaji wa mikopo ya asilimia kumi itokanayo na mapato ya ndani imetenga jumla ya Shilingi 436,416,470 kwa ajili ya
kukopesha vikundi vya wananwake, vijana na watu wenye ulemavu vitakavyokidhi vigezo vya kupatiwa mikopo ambapo mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 10.11.2024.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.