Wasimamizi wa vituo vya kupigia kura vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema wameaswa kusimamia vyema zoezi la upigaji wa kura kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba, 2024 kwa kuzingatia miongozo na sheria ya uchaguzi ili zoezi hilo likamilike kwa amani na utulivu.
Akifungua semina kwa wasimamizi wa vituo vya kupigia kura leo Novemba 23, 2024, Msimamizi wa uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Binuru Shekidele amewataka wasimamizi hao wa vituo kujiepusha na viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani siku ya uchaguzi kama vile matumizi ya lugha chafu kwa wapiga kura ambapo amewataka kuzingatia miongozo ya uchaguzi watakayopatiwa wakati wakati wa semina hiyo.
"Kafanyeni kazi hii kwa umakini na weledi mkubwa, tumieni miongozo mtakayopewa ili uchaguzi huu ukafanyike kwa haki na amani, naombeni tusiwe chanzo cha vurugu kwenye uchaguzi huu" amesema Msimamizi wa uchaguzi.
Msimamizi wa uchaguzi amesema iwapo wasimamizi hao watatenda haki na kuzingatia miongozo ya uchaguzi ni wazi kuwa uchaguzi huo utakuwa wa haki na amani.
Wasimamizi hao wa vituo vya uchaguzi wamekula kiapo cha utii na utunzaji wa siri mbele ya Kamishna wa viapo Mhe. Christopher Mbuba ambapo amewataka wasimamizi hao wa vituo kuheshimu viapo hivyo.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika tarehe 27 Novemba, 2024 ambapo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema itafanya uchaguzi kwenye jumla ya vijiji 71 na vitongoji 421 ambapo jumla ya wapiga kura 209,635 walioandikishwa wanatarajiwa kushiriki uchaguzi huo
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.