Zaidi ya Shilingi Bilioni 50 zinatarajiwa kulipwa kwa wananchi 853 wa vijiji vya Sotta na Nyabila vilivyopo kata ya Igalula Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ili kupisha shughuli za uchimbaji Madini ya Dhahabu wa Nyanzanga unaomilikiwa kwa ubia kati Kampuni ya Ore Corp Limited (84%) na Serikali ya Tanzania (16%).
Akizungumza leo Septemba 04, 2023 kwenye hafla ya uzinduzi wa ulipaji wa fidia hizo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi amewaasa wananchi hao wanaopisha ujenzi wa Mgodi huo kuhakikisha fedha wanazolipwa zinatumika vizuri ikiwemo kujenga makazi bora pamoja na kuanzisha miradi kwa ajili ya kukuza kipato cha kaya.
"Mradi huu ni mkubwa na unatarajiwa kudumu kwa zaidi ya miaka 12, mradi utachangia mambo mengi zikiwemo ajira za moja kwa moja zaidi ya 1000 za wananchi wa maeneo haya na mengine, huu ni uwekezaji mkubwa ambao unakwenda kugusa maisha yenu moja kwa moja" amesema Mhe. Makilagi.
Mhe. Makilagi amesema hatua iliyofikiwa na ulipaji wa fidia kwa wananchi ni ishara nzuri ya kuanza rasmi kwa shughuli za uchimbaji kwenye eneo hilo hivyo ni vyema wananchi hao kuchangamkia fursa kutoka mgodini hapo ambapo pia amewaasa wananchi wa Sengerema kujiandaa na fursa za kiuchumi kama vile ajira na biashara mbalimbali kutoka mgodini hapo.
Hata hivyo, ametoa wito kwa kampuni hiyo na makampuni mengine yanayofanya kazi na Mgodi kuhakikisha wanalipa ushuru wa huduma kwa Halmashauri na kodi zote za Serikali kuu kwa wakati.
Msimamizi wa miradi ya kampuni hiyo nchini Isaac Lupokela amesema Mradi wa Nyanzaga utakuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wanaozunguka Mgodi, Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema na Taifa kwa ujumla ambapo amesema fedha za kulipa fidia kwa waguswa wote 853 zipo tayari.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema Agustine Makoye amewaasa wananchi ambao bado hawajamilisha ujazaji wa mikataba hiyo kuhakikisha wanakamilisha zoezi hilo ili kutoa nafasi kwa mwekezaji huyo kufanya kazi zake kwa wakati.
Diwani wa kata ya Igalula Mhe. Faustine Shibiliti ameiomba Serikali kutumia busara wakati wa uondoaji wa wananchi hao kupisha mgodi huo ili kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza pamoja na uzingatiaji wa ajira za wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.