Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga amewataka wananchi na kamati inayosimamia ujenzi wa kituo cha Afya Kanyelele kilichopo kata ya Buzilasoga kuhakikisha wanasimamia vyema ukamilishaji wa kituo hicho ili kiweze kukamilika kwa ubora wa hali ya juu.
Akikagua maendeleo ya Ujenzi wa Kituo hicho leo ijumaa Machi 24, 2023, Mkuu wa Wilaya ameitaka kamati inayosimamia ujenzi huo kuhakikisha wanauthamini mradi huo na mingine inayoendelea kujengwa na Serikali katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wameisaidia Serikali ambayo imekuwa ikileta fedha nyingi za miradi ya maendeleo pasipo kuchangisha fedha kutoka kwa wananchi.
"Huu ni mradi wenu, simamieni vizuri, kituo hiki tunategemea kidumu kwa muda mrefu, na ninyi ndiyo watumiaji mkiona mambo hayaendi vizuri toeni taarifa" amesisitiza Mkuu wa Wilaya.
Mratibu wa TASAF wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ndugu Malisa Ndugha amesema ujenzi wa kituo hicho kwa sasa umefikia asilimia 95 kwa majengo ya OPD, wodi ya mama na watoto na Maabara ambapo pia amesema ujenzi unaoendelea ni wa Mochwari na nyumba ya mtumishi.
Kituo hicho cha afya kinajengwa kwa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na wananchi kwa zaidi ya shilingi Milioni 543 na kitakapokamilika kinatarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 1852 wa kata hiyo na maeneo ya jirani.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.