Zaidi ya wanafunzi 88,000 wenye umri wa kati ya miaka 5-14 wa shule za Msingi 111 za Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema wanatarajiwa kupatiwa dawa za kinga ya dhidi ya magonjwa ya Kichocho na Minyoo ya Tumbo.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 20 Novemba, 2023 kwenye kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi kwa ajili ya kujadili uendeshaji wa zoezi la ugawaji wa dawa hizo linalotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 23 na 24 Novemba 2023.
Akifungua kikao hicho Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri Dkt. Fredrick Mugarula kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Sengerema amesema dawa zitakazotolewa kwenye zoezi hilo ni za kawaida na zimekuwa zikitolewa mara kwa mara hivyo amewataka wajumbe wa kikao hicho kwenda kutoa elimu sahihi kwa jamii ili zoezi hilo liweze kuwa la manufaa.
Amesema kutoka na kamati hiyo kuwa na wajumbe kutoka taasisi mbalimbali pamoja na viongozi wa madhehebu ya dini ni vyema ujumbe sahihi ukafika kwa walengwa wakiwemo wazazi wa wanafuzni ili kuweza kuzuia magonjwa ya Kichocho na Minyoo ya Tumbo.
"hizi dawa ni za kawaida, ndiyo hizi hizi hutumika kwenye zahanati zetu, vituo vya afya na hospitali zetu na maduka ya dawa, hivyo hatuna budi kuzitilia mashaka kwani hazina madhara yoyote kwa binadamu" amesisitiza kaimu Mkurugenzi.
Mratibu wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Bibi Rachel Ntogwisangu amesema katika zoezi hilo shule zilizo katika kata 22 zitapata dawa ya kichocho na dawa ya minyoo ya tumbo na shule katika kata 4 zitapata dawa za minyoo ya tumbo pekee.
Mratibu huyo ameziomba shule zote za msingi kuhakikisha wanandaa chakula kwa wanafunzi wote kabla ya matumizi ya dawa hizo.
Wajumbe mbalimbali waliohudhuria kikao hicho wameuomba uongozi wa Halmashauri kupitia ofisi ya Mganga Mkuu wa Wilaya kuhakikisha walengwa wote wanapatiwa dawa hizo ili kuweza kutokomeza magonjwa yaliyokusudiwa na wamepongeza kwa kikao hicho ambacho wamesema kimesaidia kutoa elimu sahihi kwa wananchi wakiwemo waumini wa madhehebu mbalimbali.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.