Watendaji wa Kata za Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema wametakiwa kuendela kuchukua tahadhali dhidi ya ugonjwa wa Kipindupindu hususan matumizi ya vyoo na mikusanyiko kwenye misiba pamoja na kuwachukulia hatua wazazi wenye watoto ambao hawakupatiwa Chanjo ya Surua na Rubella.
Tahadhali hiyo imetolewa leo (Februari 19, 2024) kwenye kikao kazi kilichowakutanisha watendaji wa kata za Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kwa ajili ya kujadili tathimini ya Kampeni ya kitaifa ya Chanjo ya Surua na Rubella na tahadhali ya Kipindupindu.
Mkurugenzi Mtendaji amewataka Watendaji hao kubadilika na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kuondoa changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ikiwemo magonjwa ya mlipuko, ukwepaji wa Chanjo pamoja utoro shuleni.
"Nataka nipate taarifa ya watoto wote ambao hawakupatiwa Chanjo ya Surua na Rubella katika maeneo yenu na mniambie hatua gani mmechukua, watafuteni wote hadi kufikia jioni ya leo nipate taarifa hiyo" amesema Mkurugenzi Mtendaji.
Mkurugenzi Mtendaji amesema suala la kukwepa chanjo ya Surua na Rubella si la kupuuzwa kwani Serikali imetumia gharama kubwa hivyo ni vyema ijulikane sababu ya baadhi watoto katika kata za Katunguru, Kasenyi, Igalula na Nyanchenche kutokupatiwa chanjo hiyo.
Kuhusiana na tahadhali ya Kipindupindu Mkurugenzi Mtendaji amesema mbali na Serikali kupiga marufuku shughuli za matanga na chakula kwenye misiba bado kuna baadhi ya maeneo yanakiuka maagizo hayo kitendo ambacho kitasababisha kuendelea kuwepo maambukizi mapya ya ugonjwa wa Kipindupindu ambao hivi karibuni umeyaathiri baadhi ya maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.
Watendaji wa kata wamesema mojawapo ya changamoto ya kutofikiwa malengo katika maeneo yaliyotajwa ni pamoja kuhama kwa baadhi ya kaya hususan zile zilizolipwa fidia kupisha shughuli za uchimbaji wa madini katika Kijiji cha Sotta na baadhi ya maeneo yenye wavuvi.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Dkt. Fredrick Mugarula amesema ugonjwa wa Kipindupindu ni hatari na huambukiza haraka hivyo amewaomba watendaji hao kuendelea kuchukua tahadhali ili kuweza kujikinga na ugonjwa huo ambao kwa muda mfupi tangu mlipuko huo utokee Halmashauri imeweza kutumia gharama kubwa za fedha, nguvu kazi na muda katika kukabiliana na ugonjwa huo hivyo amewataka watendaji hao kuendelea kuchukua tahadhali dhidi ya ugonjwa huo.
Katika hatua nyingine Dkt. Mugarula amesema katika kampeni ya kitaifa Chanjo ya Surua na Rubella iliyooanza tarehe 15 hadi 18 Februari, 2024 Halmashauri ilikuwa na lengo la kuwafikia watoto 98,118 lakini imeweza kuwafikia watoto 100,553 sawa na asilimia 102 ya lengo
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.