Wadau wa Lishe Wilayani Sengerema wamesema ili kufikia malengo ya shughuli za Lishe katika ngazi ya Halmashauri, ni vyema ajenda ya Lishe ikawa ya kudumu katika kila mikutano ya hadhara na vikao vya ndani.
Ushauri huo umetolewa leo Ijumaa Agosti 11, wakati wa kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe uliowakutanisha watendaji wa kata za Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na baadhi ya wakuu wa Idara na vitengo vya Halmashauri.
Wajumbe hao wamesema iwapo elimu ya Lishe itatolewa kupitia mikutano mbalimbali ya hadhara na mikusanyiko mingine kila mtu atakuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na masuala ya Lishe ambapo pia wameshauri watalaamu wa Lishe washirikishwe kwenye ziara za viongozi pamoja na vikao vya ngazi ya vijiji na kata kwa lengo la kutoa elimu ya Lishe.
"Suala la lishe liguse kila kiongozi, kupitia mikutano ya hadhara elimu itolewe na si kuiachia idara ya afya pekee katika utoaji wa elimu ya Lishe" ameshauri Muuguzi Mkuu wa Wilaya ndugu Charles Manyaga.
Mtendaji wa kata ya Busisi Ndugu Adam Salumu ameshauri shule zote msingi na Sekondari kuendeleza na kuanzisha mashamba ya Viazi Lishe shuleni ili kuongeza huduma ya chakula shuleni ambayo itasaidia kuboresha Lishe ya wanafunzi pamoja na kuongeza mahudhurio shuleni.
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Ndugu Fadhili Abel ameunga mkono suala la ushirikishwaji wa wataalamu wa Lishe kwenye kila ziara za viongozi na kuzitaka shule zote za Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kuwa angalau na ekari 2 za Viazi Lishe ili kuboresha Lishe ya wanafunzi.
Awali kimkaribisha Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Dkt. Fredrick Mugarula amesema lengo la kufanya kikao cha Tathimini ya Utekelezaji wa Lishe ni pamoja na kujitathimi kulingana na Viashiria vilivyo kwenye Mkataba wa Lishe ngazi ya Halmashauri ambapo amesema Halmashauri mejipanga kuhakikisha changamoto zote zinazokabili shughuli za Lishe zinatatuliwa ili kufikia lengo.
Afisa Lishe wa Wilaya Bi. Neema Sappy amesema miongoni mwa changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa shughuli za lishe ni pamoja na baadhi ya shule kutokutoa huduma za chakula, upungufu wa vifaa vya kutathimini Hali ya Lishe kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano pamoja na upungufu wa chakula Dawa kwa ajili ya watoto wenye utapiamlo.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.