DED, Wakuu wa Idara Watoa Somo
Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema wameaswa kufanya kazi kwa bidii sambamba na kutoa ushauri ipasavyo kwa wakuu wa idara na viongozi wengine ngazi ya Wilaya ili kuweza kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi katika ngazi za vitongoji na vijiji.
Wito huo umetolewa leo na Mbunge wa jimbo la Sengerema Mhe. Hamis Tabasamu kwenye kikao cha kazi kilichojumuisha waratibu Elimu kata, watendaji wa kata, wakuu wa shule, walimu wakuu, waganga wa wafawidhi wa vituo vya afya na zahanati kilichofanyika leo (11.07.2024) Sekondari ya Sengerema.
Akiongea na watumishi hao, Mhe. Tabasamu amesema kumekuwepo na changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema zikiwemo huduma bora za afya na elimu hivyo amewataka watumishi hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii ili kupunguza changamoto hizo ambazo wakati mwingine wananchi wamekuwa wakiwasilisha moja kwa moja kupitia ofisi ya mbunge na yeye mwenyewe.
"Fanyeni kazi zenu kwa bidii, lakini hakikisheni pia mnatusaidia kwenye ukusanyaji wa mapato, ninyi ni maafisa wa Serikali shaurini juu ya mambo mbalimbali mnayoyaona hayaendi sawa kwenye maeneo yenu" amesema Mhe. Tabasamu.
Mapema akifungua kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Binuru Shekidele amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kuyafikia malengo mbalimbali yaliyowekwa na Halmashauri ikiwemo usimamizi wa mapato na miradi ya maendeleo huku akisema kuwa ataendelea kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wote wazembe na wale wanaokwamisha shughuli mbambali za Serikali.
Kupitia kikao hicho, wakuu wa idara na vitengo vya Halmashauri wamepata fursa ya kuelezea mipango yao ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali katika kila idara ambayo yanawahusu watumishi hao sambamba na usimamizi wa watumishi waliopo chini yao, usimamizi wa raslimali, miradi na ukusanyaji wa mapato.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.