Aomba Ujenzi wa Vituo vya Afya na Malambo ya Mifugo
Mbunge wa jimbo la Sengerema Mhe. Hamis Tabasamu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema miradi mingi ya maendeleo ndani ya muda mfupi ambayo imekuwa ikitekelezwa na Serikali ya awamu ya sita.
Mhe. Tabasamu ametoa shukrani hizo wakati wa ziara ya Rais Samia Wilayani Sengerema kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi.
Mhe. Tabasamu amesema Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema imekuwa ikipokea fedha nyingi za miradi ya maendeleo hivyo kuifanya Wilaya kupiga hatua kimaendeleo ndani ya muda mfupi.
Mhe. Tabasamu ametoa mfano wa baadhi ya sekta zilizopata fedha nyingi ni pamoja na sekta ya barabara ambapo hivi karibuni ujenzi wa barabara ya lami Sengerema - Buchosa utaanza, upandishwaji wa hadhi ya Barabara tano kwa kujengwa kwa kiwango cha moramu, kuridhiwa kwa ujenzi wa Barabara ya Kamanga- Sengerema kwa kiwango cha lami ambapo itajengwa kwa awamu na kwa kuanzia kilometa 10 zitajengwa pamoja na uwekaji wa taa za Barabarani katika mji wa Sengerema.
Sekta zingine zilizotajwa na Mhe. Tabasamu ni pamoja na elimu ambapo zaidi ya shilingi bilioni 6 zimeletwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema na Utekelezaji wa miradi ya Maji.
"Sengerema ni kama ndiyo imepata uhuru mhe. Rais, yaani miradi ni mingi, inazunguka kama tairi la gari" amesema mhe. Tabasamu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewashukuru mamia ya wananchi wa Sengerema waliojitokeza kumsikiliza eneo la Busisi ambapo amesema wingi wa watu hao ni ishara kuwa wamejitokeza kumshukuru.
Mhe. Samia amesema wingi wa miradi ianyoendelea kutekelezwa wilayani Sengerema ni ukamilishaji wa ahadi zilizoachwa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli hivyo ameahidi kukamilisha miradi yote kwa wakati.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa amesema ujenzi wa daraja hilo lenye urefu wa kilometa tatu unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Februari, 2024.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.