*Tahadhali yatolewa juu ya Mikopo Umiza*
*Malipo ya Uhamisho yalipwe bila upendeleo*
*Lugha mbaya kwa Walimu zakemewa*
Serikali imewahahakikishia walimu wote Wilayani Sengerema kuwa itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuhakikisha wanafanya kazi katika mazingira mazuri.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Elimu kutoka Ofisi ya Rais - TAMISEMI Dkt. Emmanuel Shindika kwenye kikao cha pamoja na walimu wa shule za Msingi na Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kilichofanyika leo (03.06.2024) Sekondari ya Sengerema.
Dkt. Shindika amesema kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa walimu ikiwemo suala la upandishwaji wa madaraja, kubadilishwa miundo, mapunjo ya mishahara, madai ya likizo, fedha za uhamisho na pamoja na lugha mbaya kwa walimu hivyo amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutatua changamoto hizi haraka ikiwemo ulipaji wa malimbikizo ya mishahara kwa walimu pamoja na watumishi wengine.
"Katika kutatua changamoto hizi wote tumpongeze mhe. Rais Samia, kuanzia tarehe 01.07. 2024 jumla ya walimu 54,000 watapanda madaraja kwa mserereko, kati yao 52,000 watapanda kwa utaratibu wa kawaida" amesema Dkt. Shindika.
Dkt. Shindika pia amewaasa walimu kuona namna ya kujiongezea kipato na kuachana na mikopo umiza ambayo imesababisha walimu wengi kuwa katika matatizo kwenye maeneo ya kazi na amewataka viongozi mbalimbali kutumia lugha za staha kwa walimu na watumishi wengine pindi wanapofika ofisini kwa ajili ya kufuatilia changamoto zao.
Afisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Martin Nkwabi amesema Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema imekuwa ikifanya vizuri kwenye taaluma pamoja na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya sekta ya elimu.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Dkt. Fredrick Mugarula amesema sekta ya elimu Wilayani Sengerema imekuwa ikifanya vizuri ikiwemo suala la ufaulu kwa shule za Msingi na Sekondari kwenye mitihani ya kitaifa ambapo umekuwa ukipanda kila mwaka.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.