Uhamasisha nyumba kwa nyumba kufanyika
Tahadhali ya Kipindupindu Yatolewa
Halmashauri ya Wilaya Sengerema leo Februari 15, 2024 imezindua rasmi kampeni ya Chanjo ya Surua na Rubella inayotarajiwa kufanyika kwa muda wa siku nne kuanzia Februari 15, 2024.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Binuru Shekidele kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Sengerema amesema katika kampeni hiyo ya Chanjo ni lazima walengwa wote 98,118 waweze kufikiwa hivyo amewaomba wazazi na walezi wenye watoto wenye umri chini ya miaka mitano kuhakikisha wanapeleka watoto kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya Chanjo ya Surua na Rubellla.
Amesema kutokana na mwitikio mdogo katika kampeni za chanjo mbalimbali kumekuwa na madhara mengi ikiwemo gharama za matibabu kwa mtu mmoja mmoja pamoja na Serikali kuwekeza gharama kubwa kwenye matibabu badala ya kutekeleza miradi mingine ya maendeleo.
"Chanjo hii inatolewa bure kabisa, niwaombe kila mmoja wenu ahakikishe anapeleka watoto kupata chanjo, usipopata Chanjo utasababisha magonjwa mengi na utaingia gharama kubwa kutibu magonjwa hayo hayo ambayo yangekingwa na Chanjo hii" amesema Mkurugenzj Mtendaji.
Mganga mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Dkt. Fredrick Mugarula amesema nchi zilizoendelea zimepiga hatua kimaendeleo kutokana na matumizi sahihi ya Chanjo hivyo kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania hatuna budi kuhakikisha Chanjo hizi zinapewa kipaumbele na jamii nzima ili kujikinga na magonjwa mbalimbali pamoja na kuwa na kizazi chenye afya bora.
Mratibu wa Chanjo wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Bi. Mageni Magesa amesema Halmashauri imepokea jumla ya Chanjo 100,850 ambazo zitatumika kwenye vituo 95 vikiwemo vile kutolea huduma za afya 48 na vituo vya muda 47.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Tunyeye, Raymond Sau akiongea katika hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo amewataka wananchi wa kijiji hicho kuhakikisha wanajitokeza kupeleka walengwa wote kupatiwa Chanjo hiyo ambapo amesema yeye kwa kushirikiana na wajumbe wa Serikali ya Kijiji watafanya msako wa nyumba kwa nyumba kuhakikisha walengwa wote wanapatiwa Chanjo hiyo.
Kampeni ya Chanjo ya Surua na Rubella itafanyika nchi nzima kuanzia tarehe 15 hadi 18, Februari 2024 ambapo walengwa ni watoto wenye umri chininya miaka mitano.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.