Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza, imepongezwa kwa kupunguza hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutoka hoja 17 hadi kubaki na hoja 1 kwa mwaka 2022/2023 na kutoka hoja 22 hadi hadi kubaki na hoja 4 zilizokuwepo kwa kipindi cha nyuma pamoja na kuendelea kupata hati safi kwa miaka mitatu mfululizo.
Pongezi hizo zimetolewa leo (Juni 26, 2024) na Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwenye kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujadili taarifa ya CAG inayoishia Juni 2023 kilichofanyika kwenye ukumbi wa Sekondari ya Sengerema.
Katibu Tawala Mkoa amesema Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kwa miaka ya iliyopita ilikuwa na hoja nyingi sana za CAG hivyo ameupongeza uongozi wa Halmashauri kwa kujibu hoja hizo na hatimaye kubakiza hoja chache ambazo nazo zinaweza kufutwa kama maoni ya mkaguzi yakifanyiwa kazi vizuri.
"Tuna hoja chache sana zilizobaki, kipindi cha nyuma kulikuwa na hoja nyingi sana mmetoa vielelezo hoja zimefutwa ninawapongeza sana kwa jitihada hizi kwani hizi hoja zinaelekea kuisha kabisa' Amesema Katibu Tawala Mkoa.
Mapema akiwasilisha taarifa ya CAG kwenye kikao hicho, Sapensia George amesema kutokana na ukaguzi uliofanyika katika kipindi kinachoishia Juni 2023 Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ilipata hati inayoridhisha ambapo pia imefanikiwa kupata hati inayoridhisha kwa miaka mitatu mfululizo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema, Mark Agustine Makoye ameupongeza uongozi wa Halmashauri kwa kuendelea kusimamia vyema maagizo ya Serikali ambapo imesababisha kupungua kwa hoja za CAG pamoja na kupiga hatua kwenye miradi ya maendeleo.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Nganga amesema kumekuwepo na juhudi kubwa kutoka kwa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema katika kujibu hoja za CAG hivyo amepongeza kwa jitihada hizo sambamba na juhudi za ukusanyaji wa mapato ndani ambapo Halmashauri imefikia asilimia 86 ambapo ameiagiza Halmashauri kuendelea kupunguza madeni mbalimbali ya wazabuni wanaoidai Halmashauri.
Akifunga kikao hicho mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Yanga Makaga amesema kupitia kamati ya Fedha ya Halmashauri pamoja na Baraza la madiwani kwa ujumla wataendelea kuweka mikakati kwa ajili ya kudhibiti uibukaji wa hoja mpya, hivyo amewataka watumishi wa Halmashauri kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.