Halmashauri yapongezwa kusimamia vyema malengo ya BOOST na SEQUIP
Na: Richard Bagolele
Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema itanufaika na ujenzi wa shule mbili mpya za Msingi na Sekondari kupitia Mpango wa Kuimarisha na Kuboresha Elimu ya Msingi nchini (BOOST) na Mpango wa Maendeleo wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) inayofadhiliwa na Benki ya dunia.
Hayo yamebainishwa tarehe 21 Machi, 2023 na timu ya ufuatiliaji kutoka Benki ya Dunia, TAMISEMI na Wizara ya Elimu wakati wa ziara ya siku moja ya kukagua maendeleo ya Mpango wa BOOST na SEQUIP kwa shule za Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.
Kupitia ziara hiyo, Mkurugenzi wa Elimu ya Awali na Msingi kutoka TAMISEMI ndugu Susana Nyarubamba ameuagiza uongozi wa kata ya Misheni na Nyampulukano mahali ambapo shule hizo zinajengwa, kuhakikisha miradi hiyo inajengwa kwa kufuata taratibu pamoja na ushirikishwaji wa wadau wote mhimu ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa.
"Niwaombe ndugu zangu tufanye kazi kwa kushirikiana pindi miradi hii itakapoanza, asiwepo mtu wa kufanya kazi peke yake, tuzingatie maelekezo bila kukiuka taratibu, tufuate miongozo na maelekezo ya Serikali, tusipunguze thamani na ubora wa miradi hii" amesisitiza ndugu Nyarubamba.
Naye mwakilishi wa Benki ya Dunia ndugu Innocent Mulindwa mbali na kupongeza usimamiaji mzuri wa malengo ya BOOST na SEQUIP ameuasa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kuhakikisha wanaunga mkono juhudi za Serikali kupitia miradi hiyo kwa kusimamia vyema miradi hiyo ili thamani ya fedha iweze kuonekana.
Awali akisoma taarifa ya Halmashauri, Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi ndugu Donati Bunonos amesema Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema inaendelea kutekeleza mpango wa BOOST na SEQUIP kupitia mpango wa mafunzo kazini kwa walimu wote (MEWAKA), ambapo kila shule imetenga masaa mawili kwa wiki lengo ikiwa ni kujengeana uwezo na umahiri wa kufundisha mada mbalimbali za masomo zinazoonekana kuwa na changamoto.
Kupitia mradi wa SEQUIP Halmashauri pia umefanikiwa kujenga shule mpya ya Sekondari ya Ibondo na vituo viwili vya mafunzo nje ya mfumo rasmi (AEPW) pamoja na utekelezaji wa mpango wa shule salama kwa shule zote za Sekondari.
Mpango wa BOOST na SEQUIP inatekelezwa katika Halmashauri zote nchini ikiwa na lengo la kuboresha na kuimarisha miondombinu ya shule, kuboresha mafunzo kazini ya walimu, kuongeza vifaa vya kufundishia na maabara.
Timu hiyo ya ufuatiliaji imetembelea shule ya Msingi Pambalu, Sekondari ya Ibondo, TRC Sengerema,Sekondari ya Nyampulukano, pamoja na maeneo ambapo shule mpya ya Sekondari ya kata ya Misheni itajengwa na kijiji cha Mwabayanda ambako kutajengwa shule mpya ya msingi kupitia mpango wa BOOST.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.