Ukarabati wa shule 7 za Msingi kukamilika
Jumla ya shule mpya 11 za Sekondari zinazoendelea kujengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema zinatarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2024 na kuanza kutumika Januari 2025.
Akikagua maendeleo ya ujenzi wa shule hizo pamoja na ukarabati wa shule za msingi leo (Julai 23, 2024), Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Binuru Shekidele amesema kukamilika kwa shule kutasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani sambamba na kupunguza umbali kwa wanafunzi waliokuwa wanasoma mbali ambapo kukamilika kwa shule hizo kutapunguza tatizo la umbali pamoja na utoro kwa wanafunzi.
Miongoni mwa shule zilizotembelewa ni pamoja na ujenzi wa Sekondari mpya ya Sogoso iliyopo kata ya Sima, na Igaka kata ya Buzilasoga ambazo zinatarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2024 ambapo kukamilika kwa shule hizi kutaifanya Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kuwa na shule 46 za Sekondari.
Shule zingine mpya za Sekondari ambazo zinaendelea kukamilishwa ni pamoja na Igulumuki, Isole, Chamabanda, Busulwangili, Kagunga, Nyitundu, Balatogwa, Kabusuri na Ilekanilo ambazo zinajengwa kwa fedha za Serikali kuu na baadhi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania.
Aidha katika ziara hiyo Mkurugenzi Mtendaji aliyeambatana na baadhi ya wakuu wa idara, waamekagua maendeleo ya ukamilishaji wa madarasa katika Sekondari ya Ibisabageni, shule ya msingi Sogoso na Pambalu ambazo zimepata fedha kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).
Katika ziara hiyo Mkurugenzi alipata nafasi ya kuongea na walimu wa Sekondari ya Ibisabageni ambapo amepongeza uongozi wa shule hiyo kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo ambapo pia amewataka walimu shuleni hapo kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuinua kiwango cha taaluma katika shule za Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.
Kupitia kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji amewaahidi watumishi wakiwemo walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema wenye sifa na vigezo vya kupanda madaraja watapanda bila kuwepo na upendeleo.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.