Mkuu wa Wilaya atoa siku 5 wazazi kupelekea watoto shule
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Kigoma Malima ametimiza ahadi yake ya fedha taslimu na mifuko 20 ya Saruji kwa wananchi wa kijiji cha Mami kilichopo kata ya Kishinda Wilayani hapa.
Akikabidhi fedha hizo shilingi laki 7 (laki 5 za Mkuu wa Mkoa, laki 1 kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya na laki 1 kutoka kwa mdau wa maendeleo wa Kishinda) leo tarehe 08 Machi, 2023 kwa wananchi hao, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga amewapongeza wananchi hao kwa kujitolea kuchangia nguvu kazi kwenye miradi mbalimbali ambapo amesema kwa kufanya hivyo kutasaidia miradi inayopelekwa katika eneo hilo kukamilika pasipokuwa na migogoro.
"Hiki mnachokifanya cha kujitolea ni kitu kizuri sana na cha kuigwa, ukichangia kwenye miradi ya maendeleo unakuwa na uchungu na mradi huo kwa sababu umechangia na mradi utauthamini" amesema Mkuu wa Wilaya.
Kwa upande mwingine Mkuu wa Wilaya ametoa siku 5 kwa mtendaji wa kata ya Kishinda kuhakikisha anawakamata wazazi wa watoto wote ambao hawajajiunga kidato cha kwanza katika shule za Sekondari Kishinda na Tunyenye akishindwa kufanya hivyo hatua kali zitachukuliwa kwa mtendaji huyo.
Diwani wa kata ya Kishinda Mhe. Vicent Shokolo ameipongeza Serikali kwa kupeleka miradi mingi katika kata hiyo ambapo amemhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Sengerema kuwa, miradi yote itakayopelekwa katika kata hiyo wananchi wapo tayari kuchangia nguvu kazi kwani wanathamini jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali katika kupeleka miradi ya maendeleo katika kata hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Binuru Shekidele amewapongeza wananchi wa kijiji cha Mami kwa kujitolea kuchimba mtaro kwa ajili ya kupeleka maji katika zahanati ya kijiji hicho ambapo amewaomba kuendelea na moyo huo wa kujitolea kwa miradi mingine.
Akiwa katika ziara yake Wilayani hapa tarehe 1 Machi, 2023 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima aliahidi kuchangia shilingi laki 5 kwa ajili ya chakula cha wananchi wa kijiji cha Mami waliojitolea kuchimba mtaro wa kupitisha bomba la maji linalopeleka maji kwenye zahanati ya kijiji cha Mami pamoja na mifuko 20 ya Saruji kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika shule ya Msingi Mami.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.