Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilayani hapa kuhakikisha huduma za Maji ya uhakika zinapatikana kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya pamoja na taasisi zote za elimu ili kupunguza adha kwa watoa huduma, wagonjwa, wanafunzi wa bweni pamoja wananchi wanaozunguka taasisi hizo.
Akikagua maendeleo ya Ujenzi wa Kituo cha afya Kanyelele kilichopo kata ya Buzilasoga kinachotarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 1852 chini ya Mpango wa kunusuru Kaya Masikini (TASAF III) kwa zaidi ya Milioni 543, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amesema huduma za afya haziwezi kutolewa pasipo kuwepo na huduma ya maji ya uhakika hivyo ameagiza kutengwe fedha ili kuchimba kisima kirefu kitakachosaidia kituo hicho pindi kitakapo anza kutoa huduma pamoja na wananchi wanaozunguka eneo hilo.
"Kituo cha Afya bila huduma za maji haiwezekani na tusidanganyane na kutegemea Chanzo cha Maji ya mvua badala yake naomba Halmashauri itenge angalau Milioni 30 hapa ili tupate kisima kirefu cha Maji kwenye kituo hiki." Amesema mhe. Malima.
Aidha, mhe. Malima ameuagiza uongozi wa Halmashauri kuona namna kuongeza muda wa kufanya kazi na wafanyakazi kwenye kituo hicho ili kiweze kukamilika ifikapo Machi 15, 2023 ambapo amesema kukamilika kwa wakati kwa mradi huo pamoja na mingine ya TASAF kutasaidia kutimiza vigezo vya kuendelea kupata ufadhili wa miradi mingine ya maendeleo.
Mratibu wa TASAF wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ndugu Malisa Ndugha amesema ujenzi wa kituo hicho cha Afya Kanyelele umefikia Asilimia 80 na kinatarajiwa kuukamilika ifikapo Machi 10, 2023.
Miradi mingine iliyotembelewa na Mkuu wa Mkoa ni pamoja na Zahanati ya Mami, Shamba la mkulima mwezeshaji wa Pamba la ndugu Maneno Lukubanija wa Buyagu, Ukaguzi wa eneo la makazi ya wananchi watakaopisha eneo la Mgodi wa Nyanzaga, ujenzi wa vyumba saba vya madarasa Sekondari ya Ngoma pamoja na mkutano wa hadhara na wananchi wa Ngoma.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.