Asisitiza nidhamu kazini na Ukusanyaji wa Mapato
Na: Richard Bagolele - Sengerema
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Amos Makalla amewataka watumishi wa Serikali Wilayani Sengerema kufanya kazi kwa kushirikiana na viongozi wa kisiasa ili kuharakisha maendeleo.
Mhe. Makalla ametoa agizo hilo leo wakati wa ziara ya kujitambulisha wilayani hapa ambayo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, dini, wazee maarufu, wafanyabiashara pamoja na watumishi wa umma.
Mhe. Makala amesema kufanya kazi kwa ushirikiano na uwepo wa mahusiano mazuri baina ya watumishi na viongozi wa kisiasa husaidia kuondoa migogoro kazini na migawanyiko, hivyo ni vyema kila mmoja athamini uwepo wa mwingine kwani lengo ni kuleta maendeleo kwa wananchi.
"Sisi wote lengo letu ni kuijenga Sengerema kwa umoja wetu, watendaji toeni ushirikiano kwa madiwani na viongozi wengine wa siasa vile vile wanasiasa fanyeni hivyo kwa watumishi, ili tusonge mbele kwani sisi wote tunategemeana na tunatekeleza Ilani moja" amesisitiza Mhe. Makalla.
Kwa upande mwingine Mhe. Makalla amewataka watumishi wa umma wilayani hapa kufanya kazi kwa nidhamu ikiwemo matumizi mazuri ya muda, huduma bora kwa wananchi na utatuaji kero mbalimbali za wananchi kwa wakati.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga amesema Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema inayo miradi mingi ambayo inaendelea kutekelezwa ikiwemo ya sekta ya elimu na afya hivyo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa wingi wa miradi ambapo amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutaifanya Sengerema kuwa ya mfano kwa maendeleo.
"Sisi tunamshukuru sana Mhe. Rais, tuna miradi mingi ambayo inakwenda kuifungua Sengerema kama vile mradi wa Daraja la Kigongo-Busisi, Barabara ya lami Sengerema - Buchosa, Mgodi wa Nyanzanga ambapo kukamilika kwake kutaiweka Sengerema kwenye sehemu ya juu sana na tutahakikisha tunaimarisha makusanyo ya mapato ya ndani" amesema Mhe. Ngaga.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Sengerema Mhe. Augustine Makoye amesema Wilaya ya Sengerema inayo imani kubwa na ujio wa Mhe. Amos Makalla hivyo amemhakikishia ushirikiano wa hali ya juu katika kuchochea maendeleo.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.