Aaagiza ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Nyampulukano uanze kwa kasi kwani serikali ilishatoa fedha Milioni 200
Aagiza pia shule mpya ya SEQUIP ujenzi uendelee haraka
Aagiza Mwezi Januari shule zote mpya zitakazojengwa zianze kutoa huduma
Awataka watendaji na viongozi kushirikiana kuchapa kazi na kusahau msuguano wa nyuma
Atangaza kuanza rasmi kwa utoaji wa huduma hospitali ya Wilaya ya Mwabaluhi
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amemaliza rasmi mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miezi Sita wa wapi ujenzi wa shule mpya ya Sekondari chini ya Mradi wa Uboreshaji wa Elimu (SEQUIP) wapi ijengwe.
Mhe. Makalla ametatua mgogoro huo wakati akiongea na wananchi wa kata ya Nyampulukano eneo la FDC mlimani ambapo kabla ya kufika hapo alitembelea maeneo yote mawili yaliyopendekezwa kujengwa kwa shule hiyo mpya ya SEQUIP.
Mkuu wa mkoa amesema, kutokana na mgogoro huo kudumu kwa muda mrefu, serikali ya awamu ya sita imeona ni vyema kujenga shule mpya katika maeneo yote mawili ya Misheni na Nyampulukano ili huduma hiyo muhimu iwafikie wote.
"Serikali imetoa shilingi milioni 200 kwa ajili ya kukamilisha Miundombinu ya madarasa iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi wakati huohuo shule mpya ya SEQIP itaendelea kujengwa katika eneo lililopendekezwa lililopo kata ya Misheni." Makalla.
Vilevile, amewataka Halmashauri ya wilaya ya sengerema kuongeza kasi ya ujenzi wa shule hizo na kwa pamoja ifikapo mwezi januari 2023 zianze kutoa huduma kwa wananchi kwani wamesubiri kwa muda mrefu.
"Mimi kama Mtendaji mkuu nakushukuru sana Mhe. Mkuu wa mkoa maana tulishakwama kutokana na sintofahamu ya wapi tutajenga shule pamoja na kupokea fedha za ujenzi huo, nakuahidi mwezi januari shule hii itaanza na sasa tunafanya kazi kwa kasi", amesema Mkurugenzi Mtendaji, Binuru Shekidele.
Naye, Diwani kata ya Misheni Mhe. Francis Majumba amefafanua kuwa wananchi wa kata hiyo imepata faraja kutokana na kutatuliwa kwa kitendawili hicho na kupatikana kwa suluhu ambayo inakuja kuwatatulia adha ya kusuasua kwenye maendeleo kwenye eneo la Elimu.
Mapema asubuhi Mkuu wa Mkoa aliliagiza Shirika la Umeme wilaya Sengerema (TANESCO) kupeleka umeme kwenye shule mpya ya msingi ya Kijiweni iliyojengwa kwa zaidi ya shilingi Milioni 540 kwenye kata ya Chifunfu ambayo inakuja kuondoa kero ya msongamano wa wanafunzi kwenye shule mama ya Bugumbikiso.
Vilevile, amemtaka Mkandarasi anayejenga jengo la makao makuu ya Halmashauri ya Sengerema kukamilisha ujenzi huo ifikapo mwezi Mei 2024 kwa mujibu wa mkataba ili huduma zianze kutolewa hapo.
Halikadharika, amewakaribisha wananchi wa wilaya hiyo kupata huduma za afya zinazotolewa kwenye hospitali mpya ya wilaya hiyo iliyojengwa kwa zaidi ya Bilioni 2.8 na ameahidi kuwasiliana na mamlaka husika ili ziletwe Bilioni 1.5 za kukamilisha ujenzi kwenye hospitali hiyo.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.