Asema siku ya Septemba 18 kuwa Siku ya Uzinduzi wa kusikliza kero za wananchi
Aipongeza Serikali ya Rais Samia kuleta miradi mingi ya maendeleo Mwanza
Aunda kikosi kazi maalum cha kupokea taarifa za migogoro ya ardhi
Awataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuitangaza miradi ya maendeleo kwa wananchi
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.CPA. Amos Makalla ametangaza mkakati kamambe wa kutatua kero za wananchi Mkoani humo kwa kuwashirikisha Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi wa Halmashauri na Makatibu Tawala wa Wilaya.
Akizungumza leo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa katika kikao kazi na viongozi hao, Mhe. Makalla amesema atafanya uzinduzi huo Septemba 18 mwaka huu na kuwaagiza Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri,Makatibu Tawala wa Wilaya wahudhurie ili wapate mwongozo mzuri watakapokwenda kushughulika na kero za wananchi.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema utaratibu huo ameufanya kwenye mikoa yote aliyofanya kazi hivyo anaamini utaratibu huo kwa Mkoani Mwanza utakuwa na tija kwa Serikali kuwa karibu zaidi na wananchi.
"Nawaagiza viongozi wenzangu mara baada ya uzinduzi huo wa kusikiliza kero za wananchi,muende sehemu zenu za kazi na kuweka mpango kazi wa kuwatembelea wananchi kila kata na baadaye ziwasilishwe kwenye Halmashauri kwa kufanyiwa kazi",amesisitiza CPA Makalla.
Amesema manufaa ya kusikiliza kero hizo zinawapunguzia mzigo wananchi yakiwemo mashauri yaliyopo mahakamani yanayohusu migogoro ya ardhi na mengineyo na kusisitiza utaribu huo usiishie kusikiliza tu bali pia kutoa majibu, kushauri na mwelekeo wa jambo husika.
Amewaagiza pia watumishi wa Idara za ardhi kwenye Halmashauri waweke utaratibu wa kuwahudumia wananchi hasa migogoro ya ardhi na mipaka.
"Nimeunda kikosi kazi maalum ambacho kitapita kwenye Halmashauri zote kupata taarifa za migogoro ya ardhi niwaombe viongozi wote mtoe ushirikiano kwa kiosi kazi hiki",CPA Makalla
Ameongeza kuwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi waunde timu ya pamoja na kuitangaza bayana miradi yote ya maendeleo kwa wananchi na kusikiliza changamoto na muendelezo wa miradi hiyo na shule zote na hospitali ziwe na mipaka ili kuepuka kuingiliwa.
Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza Mkoa wa Mwanza bila kero za wananchi inawezekana na kazi hiyo ikifanyika kikamilifu itaondoa malalamiko kwa viongozi wa Kitaifa wanapofanya ziara.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.