Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewaagiza watendaji wa kata Wilayani hapa kutenga siku ya Alhamisi ya kila wiki kwa ajili ya kutatua kero na kushughulikia malalamiko mbalimbali yanayowakabili wananchi ili kupunguza kero hizo kwa wakati badala ya kusubiri viongozi wa kitaifa.
Mhe. Makala ametoa agizo hilo leo Novemba 08, 2023 alipokuwa kwenye mkutano wa kusikiliza malalamiko na utatuaji wa kero mbalimbali za wananchi wa Wilaya ya Sengerema mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya stendi ya zamani mjini Sengerema ambao umedhuriwa na wananchi mbalimbali pamoja na viongozi wa mbalimbali wa Serikali.
Mhe. Makalla Amewataka watendaji wa kata kutenga siku maalumu ya kusikiliza kero za wananchi katika ngazi ya kata ili kupunguza malalamiko kwa viongozi mbalimbali wanapotembelea Wilayani hapa.
Amesema kutokana na ongezeko la malalamiko yanayohusiana na ardhi Wilayani Sengerema ni ishara ya udhaifu wa watendaji katika kutatua malalamiko ya wananchi katika eneo husika.
"Watendaji wa kata, punguzeni matatizo ya ardhi ya mashamba, tengeni siku moja ya wiki watangazieni wananchi waje waeleze kero zao" amesema Mhe. Makalla.
Mhe. Makalla ametoa siku 14 kwa viongozi wa Wilaya ya Sengerema kuhakikisha wanajibu utekelezaji wa maelekezo yote yalitolewa kupitia mkutano huo ambapo wananchi 63 walitoa malalamiko yao.
Mapema akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga amesema ataendelea na mikutano ya kusikiliza kero za wananchi katika ngazi za kata na ameahidi kushughulikia kero zote zilizowasilishwa kupitia mkutano huo.
Huu ni mwendelezo wa mikutano ya usikilizaji na utatuaji wa kero za wananchi katika ngazi za Wilaya unaofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla ambapo kwa siku ya alhamisi Novemba 09, 2023 Mkuu wa Mkoa atakagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.