*Wazindua mradi wa Maji wa Bilioni 2.9 Chifunfu na Shule mpya ya Msingi Isamilo*
*Wapongeza Ujenzi wa Kituo cha Afya Nyamazugo*
Na; Richard Bagolele- Sengerema
Mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 umezindua, kuweka mawe ya msingi na kutembelea miradi sita yenye jumla ya shilingili bilioni 4.6 katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndg. Godfrey Eliakim Mnzava ameridhishwa na kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Kituo cha Afya Nyamazugo wilayani Sengerema kinachotekelezwa kwa thamani ya Tshs.Milioni 500 fedha kutoka Serikali kuu.
Akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi leo Oktoba 07, 2024 kiongozi huyo amewapongeza viongozi wa Halmashauri hiyo kwa usimamizi mzuri uliozaa mradi wenye ubora ukilinganisha na thamani ya fedha iliyotumika.
Ndugu Mnzava amesema Mhe. Rais ameamua kutoa fedha hizo kuwajengea wananchi wake zaidi ya 45,416 kutoka kwenye kata tatu za Nyamizeze, Kasenyi na Nyamazugo na maeneo ya jirani ili jamii iwe na uhakika wa kupata matibabu.
"Sengerema mmeitendea haki fedha iliyoletwa kwa ajili ya ujenzi huu, Mhe. Rais ameleta fedha hizi ili kuboresha huduma za afya, naomba muendelee kukamilisha ili kufika mwezi disemba huduma zianze kutolewa." Amesema ndugu Mnzava.
Mwenge wa uhuru 2024 pia umezindua mradi wa maji ya bomba katika kijiji cha Chifunfu wenye thamani ya Bilioni 2.9 fedha kutoka mpango wa maendeleo ya Maji (WSDP) uliotekelezwa na mkandarasi Emirate Builders Co. Ltd ambapo kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru amewaaguza RUWASA kuongea vituo vya kutekea maji ili wananchi wote 31,423 katika vijiji vya Chifunfu, Lukumbi na Nyakahako wapate huduma ya maji.
Mbunge wa jimbo la Sengerema Mhe. Hamis Tabasamu amesema kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema imetekeleza miradi mingi ya maji ambapo karibu maeneo yote ya Sengerema yatapata huduma ya maji.
Amesema kukamilika kwa mradi wa maji wa Chifunfu kunawafanya wananchi wa Chifunfu kuwa na amani hususan katika suala zima la upatikanaji wa huduma ya maji ambapo ameomba kutatuliwa kwa tatizo la maji katika vitongoji vitano vilivyosalia katika eneo hilo.
Mwenge wa uhuru ukiwa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema umezindua shule ya mpya ya Msingi Isamilo, na kutembelea mradi wa vijana wa uoteshaji wa miti na mradi wa uhifadhi wa mazingira sekondari ya Ibondo, pamoja na kujionea utoaji wa huduma za afya kwenye hospitali ya Halmashauri iliyipo Mwabaluhi.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.