Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza kupitia fedha za mapato ya ndani imetoa Mkopo wa Shilingi Milioni 73 kwa vikundi 19 vya Wanawake shilingi milioni 42.5, Vijana shilingi milioni 25 na Wenye ulemavu shilingi milioni 6.5 vinavyojishughulisha na shughuli mbalimbali za ujasiriamali.
Akifungua mafunzo kwa vikundi vilivyonufaika na Mkopo huo leo (jumanne tarehe17 Januari, 2023) ndugu Boniphace Kasasiro kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji amesema mikopo hiyo isiyo na riba imetolewa na Halmashauri kwa vikundi hivyo kwa kufuata vigezo vyote, hivyo amewaomba wanavikundi hao kwenda kuitumia vyema kama ikivyokusudiwa na iweze kutimiza malengo ya wanavikundi hao.
"Tunavyo vikundi vingi vilivyosajiliwa katika Halmashauri yetu ambavyo viliomba Mkopo huu, hivyo ni vyema na ninyi mkirejesha mikopo hii kwa wakati ili vikundi vingine pia viweze kunufaika kama ninyi" amesema ndugu Kasasiro
Mapema akimkaribisha Mkurugenzi Mtendaji kwenye mafunzo hayo, Mwenyekiti wa jukwaa la Wanawake Sengerema Bibi Daling Matonange ameishukuru Halmshauri ya Wilaya ya Sengerema kwa kuongeza kiwango cha mkopo kwa vikundi hivyo ukilinganisha na kipindi kilichopita ambapo itavisaidia vikundi hivyo kufikia malengo na ndoto zao za kuwa wafanyabiashara wakubwa pamoja na kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu.
Baadhi ya wanavikundi walionufaika na mkopo huo wameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kwa kutoa mikopo hiyo sambamba na kuwapa mafunzo ya namna bora ya kutumia fedha hizo kwani hapo awali waliogopa kuchukua mikopo hiyo kutokana na kutokuwa na elimu ya uelewa hivyo mafunzo hayo yatawasaidia kusimamia vyema fedha hizo pamoja na kufanya marejesho kwa wakati.
"Nimepata Mkopo kwa mara ya kwanza, kwa kiasi kikubwa mkopo huu umenimeongezea mtaji wangu ambao ulikuwa kidogo sana" amesema ndugu Sanifu Tanzania ambaye ni mnufaika kupitia kundi la wenye ulemavu.
Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imepanga kutoa mikopo isiyokuwa na riba zaidi ya shilingi milioni 176 itokanayo na asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa vikundi mbalimbali vya wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.