Jumla ya shilingi 584,280,028 zilizotolewa na Serikali kupitia mradi wa Mpango wa Maendeleo wa kuboresha elimu Sekondari (SEQUIP) zimekamilisha ujenzi wa shule mpya ya Misheni yenye miundombinu mbalimbali ikiwemo Madarasa, Maabara, Jengo la Utawala na Vyoo.
Akikagua maendeleo ya ujenzi ya shule hiyo leo Februari 19, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Binuru Shekidele amewataka wazazi na walezi wote wenye watoto waliochaguliwa kujiunga shuleni hapo kuhakikisha wanapeleka watoto hao katika shule hiyo ili thamani na uwepo wa shule hiyo yenye kila kitu iweze kuonekana.
Kupitia ziara hiyo Mkurugenzi Mtendaji amewapongeza walimu wote wa Sekondari za Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kwa kazi nzuri iliyopelekea matokeo mazuri ya kidato cha nne 2023 ambapo Halmashauri ilifanya vizuri kwa kuongeza ufaulu na baadhi ya shule kufuta daraja sifuri.
"Matokeo haya ni jitihada zetu sote, nilitamani nikutane na walimu wote kwani mmefanya vizuri, haya matokeo yawe chachu ya kuandaa matokeo mengine mazuri zaidi" amesema Mkurugenzi Mtendaji.
Mkurugenzi Mtendaji pia amewataka walimu wa shule hiyo kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii na ushirikiano ili shule hiyo iweze kufanya vizuri kitaaluma ambapo amesema kwa kufanya vizuri kutaleta sifa kwa Halmashauri na kwa kila mwalimu.
Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari, Genoveva Chuchuba amewata walimu waliohamishiwa katika shule hiyo kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii ili waweze kuacha alama kwani shule hiyo imejengwa vizuri na ni shule ya mfano kwa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.
Akikagua ujenzi wa shule hiyo mwezi Januari 2024 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla aliipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kwa kukamilisha ujenzi wa shule hiyo ndani ya muda mfupi na kwa kiwango cha kizuri kinyume na matarajio ya wengi.
Ujenzi wa shule hiyo ulianza mwezi Novemba 2023 na ulikamilika mwezi Januari 2024 na tayari shule hiyo imeanza kufanya kazi.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.