Wananchi wilayani Sengerema mkoani Mwanza wametakiwa kujivunia kwa maendeleo yaliyopatikana wilayani humo ukilinganisha na kabla ya uhuru ambapo kulikuwa na changamoto nyingi za kimaendeleo.
Hayo yameelezwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga wakati wa maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru yaliyofanyika sekondari ya Sengerema ambapo pia yameenda sambamba na kongamano la wazi lililowashirikisha viongozi mbalimbali wa serikali, madhehebu ya dini, wazee maarufu na wananchi wa Sengerema.
Mhe. Ngaga amesema kabla ya Uhuru Wilaya ya Sengerema haikuwa na shule ya sekondari lakini kwa sasa kuna shule za sekondari 43, shule za msingi zilikuwa 22 lakini kwa sasa kuna shule za msingi 110.
Ameongeza kusema Serikali imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo ile ya sekta za Nishati, Maji, afya, barabara na maendeleo ya jamii.
"Tunayo miradi mingi mikubwa ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa nchini kote, ikiwemo ndani ya Wilaya yetu, ikiwemo daraja la Busisi, daraja hili likikamilika litapunguza kero nyingi, haya ndiyo maendeleo tuliyokuwa tunatafuta baada ya kupata uhuru, tuna kila sababu ya kumpongeza Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan." amesisitiza Mhe. Ngaga.
Meneja wa wakala wa Barabara za vijijini na mijini (TARURA) Wilaya ya Sengerema mhandisi Prosper Francis amesema kabla ya uhuru Wilaya ya Sengerema haikuwa na mtandao wa barabara unaoeleweka bali kulikuwa na njia ndogo ndogo za waenda kwa miguu lakini kwa sasa Wilaya Sengerema ina mtandao wa barabara zenye urefu wa kilomita 2,709.
Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Sengerema Mhandisi Musa Bujiku amesema hapo awali maji katika mji wa Sengerema yalikuwa yanatoka kwa mgao kwa sasa Wilaya inajivunia kwa kupata miradi mingi ya maji ambapo amesema kwa mwaka huu wa fedha serikali imetoa kiasi cha bilioni 47 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji ambayo inatarajiwa kukamilika mwaka 2023 ambapo upatijanaji wa maji vijijini utapanda kutokana asilimia 57 asilimia 85.
Maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru yamefanyika Sekondari ya Sengerema na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na madhehebu ya dini pamoja na wananchi.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni Miaka 61 ya Uhuru, Amani na Umoja ndiyo nguzo ya maemdeleo yetu.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.