Waahidi kutengeneza Madawati 160 na kutoa miche ya Miti
Jamii Wilayani Sengerema imeaswa kuithamini na kuitunza miradi mbalimbali iliyopo katika maeneo yao ili iweze kudumu na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Wito huo umetolewa leo tarehe 27 Septemba, 2023 na Katibu Tawala Wilaya ya Sengerema Ndugu Cuthbert Midala kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya katika Hafla ya kukabidhi vyumba vinne vya Madarasa na ofisi mbili za walimu zilizojengwa kwa ushirikiano wa wananchi na kampuni ya Sotta Mining inayojishughulisha na uchimbaji wa Dhahabu katika Mgodi wa Nyazanga Hafla iliyofanyika kijiji cha Lubungo kata ya Igalula.
Amesema kumekuwa na miradi mingi inayotekelezwa na Serikali lakini imekuwa ikitelekezwa na jamii hivyo amewaasa wananchi hao kuhakikisha wanailinda vyema miradi hiyo ili iweze kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Katibu Tawala amempongeza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mhe. Mbunge wa Sengerema Hamis Tabasamu, Kampuni ya Sotta Mining na Wananchi wa Lubungo kwa kufanikisha ukamilishaji wa miundombinu hiyo.
"Miundombinu hii tusipoitunza tutakuwa tumejiadhibu sisi wenyewe maana ipo hapa kwa ajili yetu hivyo tuilinde kwa nguvu zote" amesisitiza Katibu Tawala Wilaya ya Sengerema.
Mkuu wa kampuni ya Sotta Mining ndugu Isaack Lupokela amesema katika kuboresha elimu, wadau mbalimbali wanayo nafasi kubwa kufanikisha, hivyo Sotta Mining imeona ni vyema ishirikiane na wananchi kupitia sekta ya elimu kwani ni jukumu linalogusa kila mdau wa maendeleo.
Amewaasa wananchi wa Lubungo kuhakikisha wanapeleka watoto shule kwani ndiyo haki yao msingi sambamba na kufuatilia maendeleo ya wanafunzi hao.
Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari ndugu Genoveva Chuchuba ameishukuru kampuni hiyo na wananchi kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa na ofisi ya walimu ambapo amewaomba wazazi kijijini hapo kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika malezi ya watoto pamoja na kupeleka watoto katika shule hiyo ikiwa ni sehemu ya shukrani kwa kampuni hiyo. Amesema kukamilika kwa shule hiyo kutasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi Sekondari ya Ngoma yenye jumla ya wanafunzi 1,220.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Meneja Mahusiano wa Kampuni ya Sotta Mininng ndugu Bwana amesema ujenzi wa mradi huo umejengwa kwa ushirikiano na wananchi ambapo ukamilishaji wa ujenzi madarasa hayo umejengwa kikundi cha wajasiriamali kilichopo Kijiji cha Ngoma kwa gharama ya shilingi milioni 38.
Diwani wa kata ya Igalula Mhe. Faustine Shibiliti ameishukuru kampuni ya Sotta Mining kwa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na ofisi mbili za walimu ambapo amesema kukamilika kwa shule hiyo kutasaidia kupunguza utoro na na mimba kwa wananfunzi kike hasa katika vijiji vya Lubungo na Nyasigu ambapo kuna umabali wa kilometa 8 kufika Sekondari ya Ngoma. Mhe. Shibiliti ameiomba kampuni hiyo kuwezesha pia upatikanaji wa madawati pamoja na vyoo katika shule hiyo ili iweze kuanza kwa wakati.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.