Katika kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania Bara Wilaya ya Sengerema Mkoani Mwanza imezindua rasmi zoezi la upandaji wa miti lenye lengo kuhifadhi mazingira katika maeneo yote ya Wilaya.
Akizindua zoezi hilo ambalo limeandaliwa na Shirikisho la walimu ambao ni makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Sengerema Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga amewaagiza wananchi wote pamoja na taasisi zote zilizopo wilayani hapa kuhakisha zinapanda miti hususani ile ya matunda katika maeneo yao ili kuhifadhi mazingira na kuboresha afya.
"Tupandeni miti ili tukabiliane na haya mabadiliko ya tabia ya nchi, mwenendo wetu wa ukataji miti hauendi sambamba na upandaji wa miti, hivyo tuhakikishe tuapanda miti ili tuweke vizuri mazingira yetu" alisisitiza Mhe. Nganga.
Aidha Mhe. Nganga amesema lengo la Wilaya ni kupanda miti isiyopungua milioni moja na nusu kwa mwaka hivyo ni vyema kwa wananchi wote kuongeza kasi ya upandaji wa miti ili kufikia lengo hilo. Amesema katika kuadhimisha miaka 61 ya uhuru tarehe 9 Disemba 2022 pamoja na matukio mengine Wilaya ya Sengerema itaendeleza zoezi la upandaji wa miti kwa kushirikiana na TFS ili kifikia lengo la kupanda miti zaidi ya milioni moja na nusu kwa mwaka.
Mwenyekiti wa shirikisho la walimu ambao ni makada wa CCM Wilaya ya Sengerema Mwalimu Sylivesta Sama amesema wataendelea na zoezi la upandaji wa miti pamoja na uhifadhi wa mazingira katika maeneo yote ya Wilaya ya Sengerema ikiwemo barabara ya kutoka Busisi hadi Geita hivyo ameomba wananchi wa maeneo husika kuitunza ili isiharibiwe na mifugo.
Zoezi la upandaji wa miti limezinduliwa kwa kupanda miti zaidi ya 1,800 kwenye chuo cha VETA Sengerema.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.