Mapato ya Ndani Kukamilisha Ujenzi wa Madarasa Kamanga na Ofisi ya Kata Ibondo
Bilioni 1.3 Kukamilisha Jengo la Utawala Machi 2025
Na; Richard Bagolele- Sengerema
Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema imelipongeza shirika la CEDAR kutoka Australia kwa ufadhili wa ujenzi wa ukuta wa kuzuia maji kutoka ziwa Viktoria pamoja na jitihada za shirika hilo kukiimarisha kituo cha afya Kamanga.
Shukrani hizo zimetolewa leo Novemba 12, 2024 na wajunbe wa kamati hiyo wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2024.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Mhe. Yanga Makaga ambaye pia ni diwani wa kata Nyamatongo amelishukuru shirika hilo kwa ufadhili wa mara kwa mara pamoja na ujenzi wa ukuta huo ambapo amesema kujengwa kwake kutakinusuru kituo hicho ambacho kimekuwa kikiathiriwa na maji ya Ziwa Viktoria na kusababisha kusitishwa kwa huduma pamoja na kuathiri makazi ya watumishi wa kituo hicho.
"kujengwa kwa ukuta huu kutasaidia sana kukinusuru kituo hiki kujaa maji mara kwa mara kutoka ziwani, ujenzi huu ni wa gharama kubwa bila ninyi Halmashauri tusingeweza kujenga ukuta huu kwani ni gharama kubwa" amesema Mwenyekiti wa Halmashauri.
Akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa ukuta huo unaojengwa pembezoni mwa ziwa Viktoria, Msimamizi wa ujenzi kutoka shirika hilo, Musa Victor amesema utekelezaji wa mradi huo ilianza mwezi Oktoba 2024 na unatarajiwa kukamilika mwezi Januari 2025 kwa gharama za shilingi milioni 266 mradi unaojengwa na kampuni ya SIMR kutoka jijini Mwanza.
Miradi mingine iliyokaguliwa na Kamati hiyo ni pamoja na Ujenzi wa madarasa mawili na ofisi shule ya Msingi Kamanga kwa gharama ya shilingi milioni 25 fedha za mapato ya ndani ambapo wajumbe wamepongeza kamati ya ujenzi ya kijiji cha Kamanga kwa kufanikisha ujenzi huo vizuri na thamani ya fedha kuonekana. Kamati hiyo pia imekagua ujenzi wa ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Ibondo unaojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 15 fedha kutokana na mapato ya ndani.
Kamati hiyo pia imekagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Utawala lililoko Bomani ambalo liko katika hatua za upauaji na linatarajiwa kukamilika mwezi Machi 2025 ambapo mwezi Oktoba 2024, Serikali imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo hilo.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.