Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga amesema suala la mmomonyoko wa maadili linasababishwa na baadhi ya wanafamilia na viongozi kutokutimiza wajibu wao katika kuhamasisha malezi bora kwenye jamii.
Mkuu wa Wilaya ameyasema hayo leo Mei 15, 2023 kijiji cha Nyasenga kata ya Nyampande wakati wa maadhimisho ya siku ya familia Duniani yaliyofanyika kiwilaya kijijini hapo.
Mkuu wa Wilaya amesema iwapo viongozi, wazazi, walezi na watoto watatimiza wajibu kuhusu malezi bora kuanzia ngazi ya falimia suala la mmomonyoko wa maadili katika jamii litakuwa historia.
"Wazazi, watoto, wazee wetu, viongozi wa dini na Serikali, hebu tushirikiane katika hili, kila mmoja wetu asimamie maadili, suala hili ni letu sote tushirikiane kukemea maadili yasiyofaa," amesisistiza mhe DC.
Mapema akisoma taarifa ya maadhimisho hayo, Mkuu wa idara ya Mendeleo ya Jamii Yusta Mwambembe amesema maadhimisho ya siku ya familia Duniani yanafanyika yakiwa na lengo la kuwakumbusha wazazi umuhimu wa maadili mema na upendo miongoni mwa wanafamilia hususan uzingatiaji wa maadili ya kitanzania katika malezi na makuzi ya watoto.
Mkuu wa jeshi la Polisi Wilaya ya Sengerema SSP. Haji Mohamed amesema suala la mmonyoko wa maadili katika jamii linaanza vijana hivyo amewataka kubadilisha mienendo yao kwa kufanya matendo mema ambapo ameomba kufanya mikutano ili kutoa elimu ya Polisi Jamii na masuala ya ulinzi kwa ujumla.
Kwa upande wa wananchi wa kata ya Nyampande wamesema suala la mmomonyoko wa maadili katika jamii ni matokeo ya vijana kuiga tamaduni za kigeni kama vile uvaaji usiozingatia maadili ya kitanzania hivyo wameomba wazazi waungane kukemea tabia hizo zisizofaa.
Maadhimisho ya siku ya familia yameenda sambamba na fursa kwa wananchi wa Nyampande kuuliza maswali kuhusu kero mbalimbali zinazowakabili ambapo majibu yametolewa na viongozi mbalimbali waliohudhuria maadhimisho hayo.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu ni *Imarisha maadili na upendo wa familia*.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.