Madarasa Mapya 14 yenye Madawati, Jengo la Utawala na Matundu ya Vyoo kukamilika punde
Shule ya Msingi Isungang'olo iliyopo kata ya Nyatukala Wilayani hapa inatarajiwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu mipya kabla ya mhula wa pili wa masomo unaotajiwa kuanza mapema mwezi Julai 2023.
Akikagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali shuleni hapo leo Juni 30, 2023 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Binuru Shekidele ameiagiza kamati ya ujenzi ya shule hiyo kuhakikisha miundombinu yote inakamilika kwa wakati kwa kuzingatia viwango.
"Simamieni ukamilishaji huu vizuri, msimamieni fundi akabidhi madarasa yaliyojengwa vizuri na yakamilike mapema zaidi" amesisitiza Mkurugenzi Mtendaji.
Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi ndugu Donati Bunonosi amesema jumla ya madarasa 14 yenye madawati, jengo la utawala na matundu ya vyoo 11 vimejengwa shuleni hapo kwa gharama za shilingi 450,500,000 fedha kutoka Serikali Kuu Mfuko wa Maafa.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Bi. Getruda Malisa amesema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,013 ambao wamekuwa wakitumia madarasa machache kutokana na baadhi ya madarasa ya shule hiyo kuezuliwa na Mvua kubwa mwezi Novemba 2022.
Mwanafunzi Dotto Ramadhani anayesoma darasa la nne katika shule hiyo amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kupelekea fedha kujenga miundombinu mipya shuleni hapo ambapo amesema kukamilika kwa vyumba hivyo vya madarasa kutasaidia sana kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.
Shule ya Msingi Isungang'olo ilikumbwa na maafa mnano mwezi Novemba 2022 na kusababisha baadhi ya madarasa shuleni hapo kuezuliwa na mengine kubomoka. Serikali kupitia mfuko wa Maafa mwezi Aprili 2023 ilitoa kiasi cha shilingi 450,500,000 kwa ajili ya ujenzi wa Miundombinu mipya shuleni hapo ambapo ujenzi umefikia zaidi ya asilimia 90.
Miradi mingine iliyotembelewa na Mkurugenzi Mtendaji ni pamoja na ujenzi wa shule mpya ya Msingi Nyatukala kupitia mradi wa BOOST kwa gharama ya shilingi 540,300,000, na ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa shule ya Msingi Pambalu kwa gharama ya shilingi milioni 50 fedha za mapato ya ndani.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.