Kifuatia baraza la mitihani kutangaza matokeo ya kidato cha sita 2023, na sekondari ya Sengerema kufanya vizuri kwenye matokeo hayo imebainika kuwa umoja na ushirikiano baina ya walimu, Idara ya Elimu Sekondari na Menejimenti ya Halmashauri ndiyo siri ya mafanikio hayo.
Hayo yamebainishwa leo wakati wa hafla fupi ya kuwapongeza walimu hao iliyohudhuriwa na kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri Bi. Genoveva Chuchuba pamoja na Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala Bi. Christina Bunini.
Akiongea na walimu hao, Mkuu wa Idara ya Utumishi ameupongeza uongozi wa shule hiyo kwa matokeo mazuri waliyopata na kuwataka walimu hao waongeze juhudi zaidi.
"Na mimi kama afisa Raslimali watu mmenipaisha sana, naomba juhudi hizi ziendelee, Sengerema Sekondari mmefanya vizuri sana kila mtu anataka kuleta mtoto shuleni hapa" amesema Ndugu Bunini.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bi. Genoveva Chuchuba ambaye ni Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari amesema matokeo hayo mazuri yamechangiwa na maadili mazuri ya walimu wa shule hiyo hivyo amewataka kuendeleza nidhamu hiyo kwani ndiyo msingi wa mafanikio.
Mkuu wa shule ya Sekondari Sengerema Ndugu Zacharia Kahema ameushukuru uongozi wa Halmashauri na Idara ya Elimu Sekondari kwa ushirikiano anaoupata kutoka kwao ambapo amesema lengo la shule ni kupata ufaulu wa daraja la kwanza tu ikitokea bahati mbaya iwe wachache daraja la pili.
Kwa mujibu wa matokeo yalitangazwa Julai 13, 2023 na Baraza la Mitihani nchini (NECTA) Sekondari ya Sengerema iliyokuwa na wanafunzi 679 waliosajiliwa kufanya mtihani, wanafunzi 408 walipata daraja la kwanza, wanafunzi 263 daraja la pili na watano daraja la tatu.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.