Watoto watoa tahadhari matumizi ya Mitandao
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga amewataka watoto wilayani hapa kujifunza kusema hapana kwenye matukio yanayosababisha ukatili dhidi ya watoto katika jamii.
Mkuu wa Wilaya ametoa agizo hilo leo kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika kiwilaya kata ya Sima na kuhudhuriwa na mamia ya watoto na wananchi wa kata hiyo na maeneo ya jirani.
Mkuu wa Wilaya amesema matukio mengi ya ukatili dhidi ya watoto yamekuwa yakitokea kipindi cha likizo hivyo amewataka watoto hao kutimiza wajibu wao kwa kukemea na kupinga matendo ya ukatili kwa kutumia elimu ya kujitambua wanayoipata shuleni kwani matukio mengi ya ukatili yanatokea kwa sababu watoto wenyewe kukubali kutendewa tofauti na matukio ya ubakaji.
"Na ninyi wenyewe mjifunze kusema hapana kwenye matendo ya ukatili, Mkifungua shule, takwimu zinaonesha mimba zimekuwa zikiongezeka, mtoto wa Sekondari unapataje mimba? ni uzembe na kukosa nidhamu" amesema mkuu wa Wilaya.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Binuru Shekidele amesema malezi mazuri ya watoto hutoa viongozi na wananchi wazuri hivyo ameiasa jamii kuwalea watoto katika misingi ya maadili mema.
Wakisoma risala kwa Mkuu wa Wilaya, watoto hao wamewaasa watoto wengine wilayani hapa na Tanzania kwa ujumla kuchukua tahadhali dhidi ya matumizi ya mitandao ya kijamii na vifaa vya kielektroniki kwani matukio mengi ya ukatili yamekuwa yakifanyika na kuonekana kupitia mitandao hiyo hivyo wameoimba jamii na Serikali kuwakinga watoto hao dhidi ya vitendo vya ukatili mitandaoni kwani watoto ndiyo wamekuwa waathirika wakubwa.
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika hufanyika kila tarehe 16 mwezi Juni kutokana mauaji ya watoto yaliyofanywa na askari wa utawala wa Makaburu katika Kitongoji cha Soweto nchini Afrika Kusini tarehe 16 Juni, 1976. Mauaji hayo yalitokea wakati Askari hao wanazuia maandamano ya watoto waliokuwa wanapinga mfumo wa elimu ya kibaguzi iliyokuwa unatolewa na Utawala wa Makaburu. Katika kukumbuka siku hii, Umoja wa Nchi za Afrika mnamo mwaka 1991 uliweka Azimio la kuifanya siku ya tarehe 16 Juni ya kila mwaka kuwa siku maalum ya kuwaenzi mashujaa watoto waliokufa kwa ajili ya kudai haki yao ya kuendelezwa kielimu bila ubaguzi na hivyo kuitwa Siku ya Mtoto wa Afrika
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni mwaka 2023 *“Zingatia Usalama wa Mtoto katika Ulimwengu wa Kidijitali*”
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.