Asisitiza Wanawake kuungana kujikwamua kiuchumi
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga amekemea tabia ya baadhi ya wazazi kujiweka kando kwenye malezi ya watoto kitendo kinachosababisha kushuka kwa maadili katika jamii.
Mhe. Ngaga ametoa angalizo hilo kwenye maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kiwilaya kwenye viwanja vya stendi ya zamani mjini Sengerema na kuhudhuriwa na mamia ya wanawake.
Mhe. Ngaga amesema wakinamama wanalo jukumu kubwa la malezi majumbani lakini kutokana na kujihusisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi na uzalishaji mali wamesahau kujihusisha na malezi hivyo amewataka wanawake hao kutimiza majukumu yao ikiwemo kufuatilia mienendo ya watoto wawapo majumbani na mahali pengine.
"Tunajukumu kubwa la malezi ndugu zangu, ni lazima tufuatilie watoto wetu wanakutana na changamoto gani kila siku, ni lazima tufuatilie na tujue watoto wetu wanakoenda wanakutana na changamoto gani?" amesisitiza Mkuu wa Wilaya.
Aidha Mhe. Mkuu wa Wilaya amewaasa wazazi kuwa makini na matumizi ya Teknolojia kwa watoto kwani mmomonyoko wa maadili kwa kiasi kikubwa umechangiwa na matumizi mabaya ya Teknolojia ikiwemo matumizi ya simu janja kwa watoto.
Katika upande mwingine Mkuu wa Wilaya amewataka wanawake wilayani Sengerema kuhakikisha wanashirikiana katika kuinua vipato vyao kupitia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali hususan mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kupitia Halmashauri za Wilaya kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo vyenye lengo la kuwakwamua wanawake kupitia vikundi mbalimbali.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ndugu Christina Bunini akimkaribisha Mkuu wa Wilaya amewaasa wanawake hao kuhakikisha wanatimiza majukumu ya malezi ya watoto majumbani ili kuwa na jamii yenye maadili kwani akina mama wanayo nafasi kubwa ya kusimamia malezi bora katika ngazi ya familia.
Mapema akitoa taarifa ya maadhimisho hayo ndugu Boniphace Kasasiro amesema lengo la maadhimisho ya wanawake duniani ni pamoja na kufanya tathimini ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na akina mama pamoja na kubaini changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake.
Mwenyekiti wa Jukwaa la wanawake Wilayani Sengerema ndugu Daling Matonange ameiomba Serikali kupitia Halmashauri kuweza kuongeza kiwango na wigo wa mikopo kwa Burundi vya wanawake kwani vipo vikundi vingi ambavyo vinazalisha bidhaa mbalimbali ambavyo hukabiliwa na changamoto za kukosa mikopo hiyo.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.