Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amesema Daraja la JP MAGUFULI (Kigongo-Busisi), linalounganisha mkoa wa Mwanza na Geita, linatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu.
Akikagua Ujenzi wa Daraja hilo leo tarehe 24 Januari 2025 mkoani Mwanza, Waziri Ulega amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa zaidi ya shilingi bilion 611 kugharamia daraja hilo hadi sasa.
" Mheshimiwa Rais Dkt. Samia amelikuta daraja hili ujenzi wake ukiwa asilimia 25 na kiasi cha shilingi bilioni 150 zikiwa zimelipwa leo hii tuko asilimia 96.3 na zaidi ya shilingi bilioni 611 zimelipwa katika daraja hili ambalo ni refu zaidi Afrika Mashariki litawezesha watu kuvuka kwa dakika 5", amesema Waziri Ulega.
Amewapongeza wataalam wazalendo kwa kujifunza katika mradi huo na kusisitiza ujuzi walioupata ni hazina kwa Taifa na utawawezesha kupewa miradi mingine ya aina hiyo siku zijazo.
"Fanyeni kazi usiku na mchana ili kazi ikamilike mkatumike kwenye miradi mingine ya kimkakati kwani ujuzi wa sayansi na teknolojia mlioupata ndicho kipaumbele chetu", amesisitiza Ulega.
Naye Kaimu Mtendaji mkuu wa TANROADS Eng. Doroth Mtenga amesema kukamilika kwa daraja hilo lenye urefu wa km 3 na barabara unganishi km 1.6 ni ukombozi wa kijamii na kiuchumi kwa ushoroba wa ziwa Victoria kwani kutaunganisha kirahisi barabara inayoanzia Sirari-Usagara-
Geita-Bukoba hadi Mutukula na kuiunganisha na nchi za Uganda, Rwanda na Burundi kwa njia rahisi na hivyo kukuza uchumi wa watu wa kanda ya ziwa na Taifa kwa ujumla.
Daraja hilo ambalo limesanifiwa kubeba tani 160 litadumu kwa zaidi ya miaka 100 litakapokamilika.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Geita Martin Shigella na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza Michael Masanja wamemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa Daraja hilo ambalo litaleta ukombozi wa kijamii na kiuchumi kwa ukanda huo wa ziwa.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.