Ujenzi wa tawi jipya la chuo kikuu cha ardhi kinachojengwa wilayani Sengerema katika kijiji cha Karumo kata ya Nyamatongo utaanza tarehe 17 Februari 2025.
Akiongea wakati wa makabidhiano ya eneo la ujenzi wa chuo hicho kwa Mkandarasi wa mradi huo kampuni ya Comflix Engenering Ltd. Makamu Mkuu wa chuo kikuu cha Ardhi Profesa Evaristo Liwa amesema, ujenzi wa mradi huo unajengwa kupitia mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET) kwa gharama ya shilingi bilioni 16, hivyo amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa mradi huo kwa wakati.
"Ni matarajio ya Serikali kuwa, ujenzi wa mradi huu utakamilika kwa wakati na kuleta matokeo yakiyokusudiwa, hivyo nimwombe mkandarasi kuhakikisha tunamaliza ujenzi kwa wakati ili tuweze kuona matunda ya chuo hiki" amesema Prof. Liwa.
Kwa upande mwingine Prof. Liwa amewashukuru wananchi wa kata ya Nyamatongo kwa kukubali kupisha ujenzi wa chuo hicho ambapo pia ameupongeza uongozi wa Halmashauri kwa kutoa ushirikiano tangu kutambulishwa kaa mradi huo ambapo pia Hlamshauri ya Wilaya ya Sengerema imesimamia vyema zoezi la uthamini wa eneo la chuo hicho.
Naibu Makamu Mkuu wa chuo Kikuu cha Ardhi anayeshughulikia taaluma, tafiti na ushauri Prof. John Lupala amesema ujenzi wa chuo hicho kwa awamu ya kwanza utaanza na majengo matano ambayo madarasa, jengo la taaluma na ofisi, mabweni ya wanafunzi, jengo la walimu pamoja na Zahanati kwa gharama ya shilingi bilioni 16 na milioni 300 kwa muda wa miezi 15 ambapo amesema chuo hicho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kudahili wanachuo zaidi ya 2000 kwa ngazi ya shahada, diploma na cheti.
Akiongea kwa niaba ya mwenyekiti wa Halmashauri, diwani wa kata ya Nyamazugo Mhe. Enock Sengelema ameushukuru uongozi wa chuo hicho kwa kuamua kujenga tawi la chuo hicho katika wilaya ya Sengerema ambapo amesema Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema itatoa ushirikiano muda wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.