Ujenzi Kuanza Mwezi Septemba 2023 kwa gharama ya sh. Bilioni 18
Na: Richard Bagolele - Sengerema
Chuo Kikuu cha Ardhi chenye makao makuu yake jijini Dar es Salaam kinatarajia kuanza ujenzi wa tawi jipya katika kijiji cha Karumo kata ya Nyamatongo wilayani Sengerema.
Akiongea wakati wa ziara ya siku moja wilayani hapa tarehe 5 Julai, 2023 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema kuanzishwa kwa tawi la chuo kikuu cha Ardhi mkoani Mwanza hususan wilayani Sengerema kutanufaisha wananchi wengi wa kanda ya Ziwa kupitia elimu itakayotolewa chuoni hapo ambayo italenga kutatua changamoto mbalimbali hususan katika maeneo ya ardhi, ujenzi na uvuvi hivyo amewaomba wananchi wa kanda ya ziwa kuchangamkia fursa chuo hicho kitakapoanza.
Katika hatua nyingine Mhe. Prof. Mkenda amewapongeza viongozi na wananchi wa Sengerema wakiongozwa na Mbunge Hamisi Tabasamu kwa utayari wa kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa chuo kikuu hicho lakini pia kwa kuwa mstari wa mbele kuchangia katika miradi ya maendeleo hususan ujenzi wa vyumba vya madarasa.
"Niwapongeze wananchi wa Sengerema kwa utayari wenu wa kutoa eneo hili kwa ujenzi wa chuo, lakini pia kwa utayari wenu wa kuchangia katika miradi mbalimbali ya maendeleo, hii ni wilaya ya mfano" amesema Prof. Mkenda
Mapema akitoa taarifa ya ujenzi wa chuo hicho, Makamu Mkuu wa Chuo cha Ardhi Prof. Evaristo Liwa amesema ujenzi wa chuo hicho utaanza mapema mwezi Septemba 2023 na unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba 2024 kwa gharama ya shilingi bilioni 18 ikijumuisha ujenzi, vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Prof. Liwa amesema kwa kuanza chuo hicho kitafundisha masomo ya teknolojia ya ujenzi, utaalamu wa michoro ya ujenzi, utawala wa ardhi na mazingira hususan raslimali za ziwa Victoria ambapo amesema masomo hayo yote yatatolewa kwa ngazi stashahada (Diploma) ambapo chuo kitaanza na idadi ya wanachuo 350 kwa mwaka wa kwanza.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia chuo hicho kujengwa wilayani Sengerema ambapo amesema kujengwa kwa chuo hicho kutaisaidia Wilaya ya Sengerema kukua zaidi kiuchumi.
Akiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Mhe. Prof. Mkenda ametembelea chuo cha Maendeleo ya wananchi Karumo, chuo cha ufundi Sengerema kilichopo Nyatukala ambapo uongozi wa Wilaya umeomba kukabidhi chuo hicho Wizara ya Elimu kiweze kuwa chuo cha VETA na Tabaruka ambapo uongozi wa Wilaya umeomba ujenzi wa shule mpya ya ufundi.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.