Shule shikizi ya Chitandele iliyopo kata ya Chifunfu imeanzisha ujenzi wa nyumba moja ya familia mbili (two in one) kwa ajili ya walimu wa shule Hiyo inayojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kwa kushirikiana na wananchi waliopo kisiwani humo.
Akiongea na wananchi mara baada ya zoezi la uchimbaji wa msingi wa nyumba hiyo, Diwani wa kata ya Chifunfu mhe. Robert Madaha amewaomba wananchi hao kujitoa kikamilifu kwa kushiriki katika ujenzi wa nyumba hiyo kwa kuchangia nguvu kazi ili nyumba hiyo ukamilike kwa wakati na walimu waweze kuishi karibu na shule hiyo.
"Tumepata bahati ya kuletewa mradi huu wa nyumba katika eneo letu, ni jambo jema kwetu hatuna budi kujitolea kwa nguvu kazi ili tukamilishe kwa wakati.
Akiongea kwa niaba ya Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri, Ndugu Neema Sagwa amewapongeza wananchi hao kwa kujitolea nguvu kazi ambapo amesema kuongeza kwa miundombinu katika shule hiyo shikizi kutasaidia kupata vigezo kwa ajili ya kuisajili na kuwa shule kamili ya msingi hivyo amewaomba wazazi wa eneo hilo kuhakikisha wanaandikisha watoto wote waliofikisha umri wa kwenda shule.
Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ndugu Malisa Ndugha amesema ujenzi wa nyumba hiyo unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi 68,760,943 fedha kutoka TASAF pamoja na nguvu za wananchi zinazokadiriwa kufikia shilingi milioni 6. Ndugu Malisa mesema ujenzi wa nyumba hiyo unatarajiwa kukamilika ifikapo Aprili 30, 2023 hivyo amewaomba wananchi hao pamoja na kamati ya ujenzi kuhakikisha wanatanguliza uzalendo kwanza katika shughuli za ujenzi wa nyumba hiyo.
Shule shikizi ya Chitandele ina jumla ya wanafunzi 100 wa darasa la awali hadi la nne, wanafunzi 13 wa darasa la tano hadi la saba waishio kisiwani humo hulazimika kwenda kusoma shule ya msingi Lukumbi iliyopo nje ya kisiwa hicho.
Kukamilika kwa nyumba hiyo kutaisadia shule hiyo shikizi hiyo kuwa na nyumba 2 za walimu ambapo kwa sasa kuna nyumba moja ya mwalimu.
Kisiwa cha Chitandele kilichopo kijiji cha Lukumbi kata ya Chifunfu kinakadiriwa kuwa kaya 76 na wakazi 300.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.