Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima amepania kuboresha kilimo cha zao la Pamba ambapo ameagiza kuanzishwa kwa umoja wa wakulima wa Pamba Buyagu Wilayani Sengerema ili kuongeza uzalishaji na kutoa elimu kwa wakulima wa maeneo mengine.
Akizungumza na baadhi ya wakulima wa Pamba wa kata ya Buyagu alipotembelea mashamba yao ya Pamba, Mhe. Malima amesema bado wakulima wa zao hilo hawalimi kilimo cha kisasa kitendo ambacho kinarudisha nyuma uzalishaji wa zao hilo, ambapo amesema mpango wa kuanzisha kilimo cha kisasa cha zao hilo utaenda sambamba na kuongeza uzalishaji wa zao hilo ili watu wengine kutoka maeneo mengine wajifunze.
"Mimi ninataka wakulima wengine kutoka maeneo yote ya Afrika waje wajifunze Buyagu kilimo bora cha Pamba na inwezekana" amesisitiza mhe. Malima
Mkuu wa Mkoa ameiagiza Bodi ya Pamba kushirikiana na Halmashauri kuanzisha umoja wa wakulima wa Pamba wa eneo hilo pamoja na kujenga kituo maalumu cha wakulima wa Pamba kwa ajili ya kuwahudumia wakulima hao kitendo ambacho kitapelekea wakulima kuweza kukopeshwa Pembejeo.
"Mimi nawaomba, tutenge kanda hii iwe ya majaribio kwenye zao la Pamba. Tutafanya usajili wa wakulima wote, lazima tupime pia udongo huu tujue ni mbolea gani inahitajika" amesema mhe. Malima
Mhe. Malima amesema mpango huo pia utahusisha utoaji wa mikopo ya Pembejeo kwa kushirikiana na mabenki pamoja na Halmashauri kuwezesha miundombinu ya umwagiliaji pamoja na elimu ya upandaji kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo ili mkulima kwa hekari moja apate kilo angalau 2000.
Mkuu wa Mkoa amesikitishwa kutokana na kuwaona wakulima wakipoteza fursa ya kupata fedha nyingi kupitia zao la Pamba kutokana na kutokuzingatia kanuni bora za kilimo cha Pamba.
Mkuu wa Mkoa ameunda kamati maalumu inayohusisha wataalamu wa kilimo ngazi ya Wilaya na Mkoa ambapo itaandaa taarifa mhimu za wakulima hao pamoja na ukubwa wa mashamba yao.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.