Latoa Siku 7 kwa Kampuni hizo Kulipa
Kamati ya Ufuatiliaji Madai Yaundwa
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema limetoa siku saba kuanzia Agosti 23, 2024 kwa wakandarasi, wazabuni, kampuni wafanyabiashara mbalimbali wanaofanya kazi kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kuhakikisha wanalipa ushuru wa huduma vinginevyo Baraza hilo litachukua hatua za kisheria dhidi yao.
Kupitia kikao cha baraza la madiwani kilichoketi leo Agosti 23, 2024, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Mhe. Yanga Makaga amelazimika kuunda kamati ya wajumbe saba kwa ajili ya ufuatiliaji wa makampuni hayo ambayo yamekuwa yakikwepa kulipa ushuru wa huduma kwa Halmashauri kitendo kinachosababisha kutokufikia malengo ya Halamshauri kwenye ukusanyaji wa mapato.
"Waheshimiwa madiwani kwa hili hapana, tunatoa siku saba tofauti na hapo tutaitisha kikao kingine tufanye maamuzi juu ya wakandarasi hawa, na ninaunda kamati kufuatilia hili jambo" amesema Mhe. Makaga.
Diwani wa kata ya Tabaruka Mhe. Sospiter Busumabu amesema ni aibu kwa wakandarasi wanaofanya kazi kupitia wakala wa Barabara vijijini na Mjini (TARURA) kukwepa kulipa ushuru wa huduma na ameitaka TARURA iwajibike kwa kuwataka wakandarasi hao kulipa ushuru wa huduma kwa Halmashauri kwani ni takwa la kisheria.
Diwani wa kata ya Kishinda Mhe. Vicent Shokolo amesema kitendo cha kutokukusanya ushuru wa huduma kutoka wakandarasi wanaofanya kazi na na baadhi ya taasisi ikiwemo TARURA kinakera na wamemtaka Meneja wa TARURA Wilaya ya Sengerema kuhakikisha anatoa ushirikiano kwa Halmashauri kwani zote ni taasisi za Serikali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Binuru Shekidele amesema taasisi zote zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ikiwemo TARURA, SEUWASA, TANESCO na Mgodi wa Nyanzaga zimeandikiwa barua ya kukumbushia kampuni na wafanyabiashara wanaofanya kazi na taasisi hizo kuhakikisha wanalipa ushuru wa huduma kwa Halmashauri.
Mbunge wa Jimbo la Sengerema Mhe. Hamis Tabasamu ameitaka TARURA na taasisi zingine kuhakikisha zinaelekeza makampuni na wafanya biashara wanaoingia mikataba nao kuhakikisha wanalipa tozo zote za Halmashauri kwani wamekuwa wakisaini mikataba mingi na kampuni hizo, hivyo hawapaswi kukwepa kulipa ushuru wa huduma.
Kwa mujibu wa sheria ya fedha ya Serikali za Mitaa sura ya 290 na marekebisho yake ya mwaka 2019 kifungu cha 6 mfanyabiashara yeyote mwenye leseni, kampuni, wakandarasi wanaofanya kazi ndani ya Halmashauri husika wanatakiwa kulipa ushuru wa huduma kwa Halmashauri husika isiyopungua asilimia 0.3 ya mauzo ghafi.
Kupitia kikao hicho Baraza la madiwani limemchagua tena Mhe. Makoye Sengerema diwani kata ya Sima kuendelea kuwa Makamu mwenyekiti wa Halmashauri kwa kipindi cha mwaka 2024/2025 ambapo pia zimeundwa kamati mbalimbali za kudumu.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.