Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema tarehe 10 Januari, 2023 limepitisha mapendekezo ya mpango na bajeti ya mwaka 2023/2024 yenye kiasi cha shilingi 56,136,022,839.00 (Bilioni hamsini na sita, milioni miamoja thelathini na sita, elfu ishirini na mbili na mia nane thelathini na tisa bila senti) huku likisisitiza kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato.
Katika kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Yanga Makaga ameiagiza timu ya Menejimenti ya Halmashauri kuhakikisha inaweka mikakati madhubuti ya ukasanyaji wa mapato kwani bajeti pendekezwa kwa upande wa mapato ya ndani imeongezeka kwa asilimia 18 kutoka shilingi 2,749,992,000 ya mwaka 2022/2023 na kufikia shilingi 3,377,319,839.00.
"ongezeko la asilimia 18.5 la mapato ya ndani sio kidogo, Menejimenti fungeni mikanda, hatutarajii kushuka hapo, kila idara ihakikishe inakusanya mapato kwa asilimia 100" alisisitiza Mhe. Makaga huku akiwaomba madiwani hao kushirikiana na timu ya menejementi ili kufikia lengo la mapato.
Mbali na kupongeza bajeti hiyo, Baraza la Madiwani pia limeagiza menejimenti ya Halmashauri kuhakikisha wanawachukulia hatua kali wote wanaokwepa kulipa ushuru na tozo mbalimbali za Halmashauri.
Diwani wa kata ya Nyampande Mhe. George Kazungu amewaomba viongozi kuwa mfano bora kwenye ulipaji wa mapato ya Halmashauri ili iweze kufikia malengo ya kuwahudumia wananchi na amesisitiza uwepo wa takwimu sahihi za wafanayabiashara wanaotakiwa kulipa leseni za biashara katika mwaka husika.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Sengerema ndugu Jamary Athuman amelipongeza baraza hilo na timu ya menejimeti kwa ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikalia na CCM ambapo kumeifanya Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ipige hatua hivyo amelitaka baraza hilo kwenda kwa wananchi kiwaelezea mambo mazuri yanayotekelezwa na Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ndugu Binuru Shekidele amelishukuru baraza hilo kwa kukubali kupitisha mapendekezo hayo ya bajeti na ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na baraza hilo.
Mapema akiwasilisha mapendekezo ya bajeti, afisa mipango wa Halmashauri ndugu Pastory Mukaruka amesema bajeti inayopendekezwa imeongezeka kwa asilimia 1.12 kutoka shilingi 55,505,703,000.00 ya mwaka 2022/2023 na kufikia shilingi 56,136,022,839.00. Katika bajeti hiyo Mishahara ni shilingi 38,583,256,000.00, Ruzuku ya matumizi mengineyo ni shilingi 1,115,111,000.00, Ruzuku ya miradi ya maendeleo shilingi 7,025,121,000.00 na Ruzuku ya Wafadhili ya miradi ya maendeleo ni shilingi 6,032,206,000.00
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.