Stendi ya Kisasa na Soko Jipya Kujengwa Mjini Sengerema
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema leo Januari 17, 2025, limepitisha mpango na bajeti wa mwaka 2025/2026 yenye jumla ya shilingi 66,308,388,446 huku likiweka vipaumbele vya kuanzisha miradi ya kimkakati ikiwemo kituo cha mabasi na soko mjini Sengerema.
Akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Mhe. Yanga Makaga amesema kwa mwaka 2024/2025 Serikali imeweza kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kitendo ambacho kimesababisha kuanzishwa na kukamilika kwa miradi mingi katika sekta zote hivyo ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi wa Sengerema.
"Bajeti ya 2023/2024 Sengerema tulivuka lengo kwa asilimia 115, kwa bajeti tuliyonayo sasa, tupo zaidi ya asilimia 55 ya lengo la bajeti, tumpongeze sana Mhe. Rais, mbunge wetu pamoja na timu ya Menejimenti kwa jitihada za kutufikisha hapa" amesema Mhe. Makaga.
Akiwasilisha bajeti hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Mkuu wa idara ya Mipango, Wilbard Bandola amesema katika bajeti inayopendekezwa, vipaumbele ni pamoja na uanzishwaji wa miradi ya kimkakati yenye lengo la kuongeza mapato ikiwemo ujenzi wa kituo cha kisasa cha Mabasi pamoja na Soko mjini Sengerema kwa gharama ya shilingi 5,076,790,995.
Baadhi ya Madiwani wamesema kukamilika kwa daraja la Magufuli kutaisaidia Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kukua kiuchumi, hivyo miundombinu bora kama kituo cha mabasi cha kisasa na soko zuri haviepukiki na lengo likiwa ni kuimarisha shughuli za kiuchumi kwa Halmashauri ya Sengerema.
Katika bajeti hiyo Halmashauri inatarajiwa kukusanya mapato ya ndani jumla ya shilingi 3,312,209,446 ambapo fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni shilingi 17,312,559,000, amesema katika bajeti hiyo inakadiriwa kuwa na ruzuku ya mishahara yenye jumla ya shilingi 44,218,387,000 pamoja na matumizi mengineyo ya shilingi 1,465,228,000.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.