Lampongeza Mbunge Tabasamu kwa Jitihada Binafsi Kuleta Maendeleo
Idara ya Afya Yapata Watumishi wapya 104
Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema limepitisha azimio la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwa Halmashauri hiyo.
Azimio hilo la pongezi limetolewa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya kwanza kilichofanyika tarehe 15 Novemba, 2024 kwenye ukumbi wa mikutano wa Bomani.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Mhe. Yanga Makaga amesema katika kipindi cha hivi karibuni Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema imekuwa ikipokea fedha nyingi za miradi ya maendeleo kupitia sekta zote hivyo ni vyema Baraza hilo likamshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada hizo za kuwaletea maendeleo wananchi wa Sengerema na Tanzania kwa ujumla.
"Hivi karibuni tumepokea fedha nyingi kupitia sekta ya Maji, Barabara, Afya na Elimu, bado haitoshi tumepokea watumishi zaidi ya mia moja wa idara ya afya, hii ni historia kubwa kwetu" amesema Mwenyekiti wa Halmashauri.
Mbunge wa jimbo la Sengerema Mhe. Hamis Tabasamu amesema Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema imepokea fedha nyingi za miradi ya Maendeleo ukilinganisha na kipindi kipindi kingine hivyo ni vyema Baraza hilo kwa kauli moja likampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema hususan ujenzi na ukarabati wa Barabara nyingi ambazo zilikuwa hazipitiki na sasa zinapitika, miradi ya umeme, maji, afya na elimu.
Mhe. Tabasamu amesema kupitia fedha za mfuko wa jimbo, mapato ya ndani pamoja na fedha za wadau wengine zimefanikisha kujenga uwanja wa mpira wa miguu ulipo Mnadani mjini Sengerema hivyo ameomba ushirikiano huo ulipo baina ya viongozi wote uendelee ili Halmashauri iweze kufikia malengo yake kwa wakati.
Diwani wa kata ya Tabaruka Mhe. Sospter Busumabu amesema kutokana na fedha nyingi za miradi ya maendeleo ni vyema Baraza hilo likampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na miradi mingi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa katika katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri pasipo kuhusisha michango ya wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Binuru Shekidele amesema maendeleo yanayoonekana katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ni kutokana na ushirikiano ulipo baina ya viongozi ambapo amesema kutokana na ushirikiano huo umekuwa ukifanikisha mambo mbalimbali ikiwemo ukamilishaji wa miradi kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa ambapo amemshukuru mbunge wa jimbo la Sengerema kwa utayari wake katika kushughulikia kero za wananchi wa Sengerema.
Wajumbe wa Baraza hilo pia wamepongeza Mhe. Tabasamu kwa jitihada za kuwaletea maendeleo wananchi wa Sengerema ambapo wamesema kwa jitihada zake binafsi amekuwa akifuatilia mambo mbalimbali na kufanikisha hivyo kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, ubovu wa barabara, vituo vya afya na zahati, uanzishwaji wa shule mpya za msingi na sekondari pamoja na upatikanaji wa watumishi kwenye sekta ya afya na elimu.
Mwezi Oktoba Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema imepokea shilingi Bilioni 2.18 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la Utawala la Halmashauri lililopo Bomani pamoja na sekta ya elimu na afya.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.