Laipongeza Idara ya Elimu Sekondari kwa matokeo mazuri
Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema limeipongeza timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kwa kusimamia vyema zoezi ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na kusimamia vizuri upelekaji wa fedha za asilimia 40 za miradi ya maendeleo zitokanazo na mapato hayo.
Wakiongea kwa nyakati tofauti kwenye kikao cha Baraza hilo kilichofanyika leo jumatano tarehe 15 Machi, 2023, wajumbe hao wamesema kwa sasa ukusanyaji wa mapato unakwenda vizuri hivyo wameitaka timu ya Menejimenti kuhakikisha inabuni vyanzo vingine vya mapato ikiwemo uboreshaji wa stendi ya Mabasi ya Bukala na ile ya Mnadani pamoja na soko la Migombani ili kufikia lengo la ukusanyaji mapato ya ndani.
Madiwani hao wamesema kitendo cha kusimamia vyema ukusanyaji wa mapato kunarahisisha shughuli mbalimbali za Halmashauri zikiwemo za ujenzi wa miradi inayotegemea mapato ya ndani na shughuli zingine za utoaji huduma kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Mhe. Yanga Makaga amesema kwa sasa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema mambo mengi yanakwenda vizuri hivyo amewapongeza watumishi kwa kufanya kazi kwa kujituma na amewaomba madiwani kutoa ushirikiano ili kuweza kufikia malengo ikiwemo ukusanyaji wa mapato ya ndani.
"Halmashauri yetu kwa sasa imetulia, shughuli zinafanyika vizuri, ni vyema tuwe na tabia pia ya kuwapongeza watumishi wanapofanya vizuri" ameongeza kusema Mhe. Makaga.
Diwani wa kata ya Kahumulo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira mhe. Fortunatus Nzwagi amesema kuna haja ya kuipongeza Menejimenti kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani kwani kwa kufanya hivyo kumesababisha upelekaji wa fedha za miradi inayotokana na mapato ya ndani kufika kwa wakati.
Naye diwani wa kata ya Tabaruka mhe. Sospiter Busumabu amesema Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kwa sasa mambo mengi yanakwenda vizuri hivyo ameliomba Baraza hilo kumpongeza Mwenyekiti wa Halmashauri kwa usimamizi mzuri wa Halmashauri ikiwemo ukusanyaji wa mapato ya ndani na usimamizi miradi mbalimbali ya Halmashauri.
Hata hivyo diwani wa kata ya Igulumuki ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya Elimu mhe. Deus Ndaki ameipongeza Idara ya Elimu Sekondari kwa kusimamia vizuri taaluma kitendo kilichopelekea kuongezeka kwa ufaulu kwenye mtihani wa kidato cha nne 2022 na kupunguza daraja sifuri kwenye baadhi ya shule.
Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imepanga kukusanya shilingi 2,043,228,000 za mapato ya ndani, ambapo hadi sasa kufikia mwezi Februari 2023 imekusanya shilingi 1,204,751,966.19 sawa na asilimia 58.96 ya lengo la mwaka, ambapo shilingi 476,522,413.99 tayari zimetolewa kwenda kwenye miradi ya maendeleo sawa na asilimia 60.17 ya lengo.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.