ASKOFU MALASUSA ASIFU USHIRIKIANO WA KKKT NA SERIKALI
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dkt. Alex Malasusa amesifu ushirikiano baina ya madhehebu ya dini likiwemo KKKT na Serikali ambapo amesema kufanya hivyo kuna jenga mahusiano mazuri baina ya Wananchi na taasisi hizo.
Askofu Dkt. Malasusa ameyasema hayo leo Januari 21, 2025 wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani Sengerema yenye lengo la kujionea shughuli za Mradi wa USAID Kizazi Hodari Kanda ya Kaskazini Mashariki ambapo ametembelea kijiji na kata ya Igulumuki.
Dkt. Malasusa amesema kupitia shughuli nzuri za uzalishaji za vikundi kupitia mradi huo ni ishara kuwa jamii ina umoja na umoja huo unatokana na mahusiano mazuri baina ya serikali na wananchi hivyo ni vyema mahusiano hayo yakaendelezwa.
"Ushirikiano huu baina ya madhehebu ya dini na Serikali unaweza kutufikisha mbali sana, lakini pia unadumisha amani, miradi hii haibagui dini au dhehebu la mtu au itikadi za kisiasa, hivyo ni vyema tukaendeleza ushirikiano huo" amesema Askofu Dkt. Malasusa.
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema mhe. Senyi Nganga akimkaribisha Askofu Mkuu Dkt. Malasusa wilayani Sengerema amelishukuru kanisa la KKKT kwa kuleta mradi wa USAID Kizazi Hodari wilayani Sengerema ambapo amesema kupitia mradi huo ni wazi kuwa wananchi wa Sengerema watanufaika pamoja na kuisaidia Serikali katika kufikia malengo yake ambapo ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano na madhebu yote ya dini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Binuru Shekidele akitoa shukrani zake kwa Askofu Dkt. Malasusa amempongeza kupitia kanisa la KKKT kwa mradi huo katika kata ya Igulumuki ambapo amesema kupitia miradi hiyo jamii itajinasua na janga la umasikini.
Mradi wa USAID Kizazi Hodari Wilaya ya Sengerema ulianza mwezi Oktoba 2023. Lengo kuu la mradi huo ni kuboresha huduma za afya, ustawi na ulinzi na usalama kwa watoto walio katika mazingira hatarishi na katika kata ya Igulumuki mradi huo umeweza kutoa huduma kwa walengwa 77.
Sengerema District Council
Anuani ya Posta: Box 175
Simu ya Mezani: 028 2590162
Simu: 0688223308
Barua pepe: ded@sengeremadc.go.tz
Copyright ©2021 SENGEREMA DISTRICT COUNCIL . All rights reserved.